SITTA AFUNGUKA KUHUSU KUCHEZEWA KWA SAINI YA NYERERE NA MSEKWA

Mwenyekiti wa Bunge la Katiba,Samuel Sitta amekiri “kuchezewa” kwa saini ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na sehemu ya saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa zilizopo kwenye hati ya sheria ya kuridhia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Akizungumza na gazeti hili jana, Sitta alisema ni kweli kuna maneno katika hati hiyo ya sheria namba 22 ya 1964, iliyosainiwa na Nyerere na Msekwa, Aprili 25, 1964, yameongezwa.
Alisema katika saini ya Nyerere kumeongezwa herufi “us” kwa kompyuta na katika sehemu ya saini ya Msekwa kumeandikwa neno “Msekwa” kwa kompyuta, jambo ambalo ni makosa. Sitta alisema walioongeza maneno hayo ni wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kuona sehemu ya maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini walifanya makosa.
“Wale vijana walipoona document (nyaraka) haisomeki waliongeza “us” mwisho kwa kompyuta kwenye saini ya Nyerere, ila walifanya makosa maana bora kitu kionekane kufifia hivyo hivyo lakini kibaki na maana yake,” alisema.
Hata hivyo, Sitta alisema kwa waliofanya kazi na hayati Baba wa Taifa wanatambua saini iliyopo kwenye hati ya sheria hiyo ipo sawa ukiondoa makosa ya kuwekwa herufi hizo.
Kuhusu saini ya Msekwa, alisema pia kulifanyika makosa katika sehemu ya saini hiyo, kuandikwa kwa kompyuta “Msekwa”.
“Ni saini ya Msekwa, lakini vijana wa chamber kwa AG waliongeza neno “Msekwa” kwa kompyuta. Ni mtu asiyejua thamani na uhalisia wa saini ni kubaki ilivyo hata kama kwa miaka 100 hata mtu aje kuisoma kwa darubini,” alisema.
Hata hivyo, alisema maudhui ya hati ya sheria hiyo, iliyosainiwa rasmi Aprili 25, 1964 ni sahihi kama ambavyo walikubaliana waasisi wa Muungano, Nyerere na Karume.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema alisema kwamba hafahamu kama ofisi yake inahusika na kuchezewa kwa saini hizo, tofauti na madai ya Sitta.
Sheria iliyopitishwa Z’bar
Sitta alisema ili kuondoa utata, ameagiza kupatiwa hati ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume (Presidential Decree) aliyotoa kusaini makubaliano kwani wakati huo, hakukuwa na Bunge.
“Karume alitumia Baraza la Mapinduzi akatumia amri ya Rais akasaini. Tunatarajia kuipata hiyo, sasa tutakuwa tumepata nyaraka za Bara na Zanzibar,” alisema Sitta.
Hata hivyo, alisema kisheria kilichopitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la MapinduziZanzibar ni yaleyale yaliyopo kwenye mkataba wa Muungano.
“Unajua kuhoji sasa mambo haya ni kupoteza muda, ni kama kuulizana na mke wako cheti cha ndoa baada ya kuishi pamoja miaka mingi, jana (juzi) nilikuwa nawaomba wajumbe kujua tunachotakiwa ni kutengeneza Katiba ambayo, inajibu matatizo yetu,” alisema Sitta.
Hati ipo UN - Akizungumzia hati ya Muungano, alisema kuwa ni kweli kupata hati hiyo kuna umuhimu, lakini mambo yote muhimu yanayohusu Muungano yamewekwa katika sheria hizo mbili zilizoridhiwa na pande zote.
Alisema kwa muda walionao wajumbe wa bunge hilo, lazima wautumie vizuri kuliko kwenda hadi Umoja wa Mataifa (UN) kwa ajili ya kuchukua hati hizo.
“Bunge la Tanganyika lililetewa muswada unaoonyesha mambo waliyokubaliana Nyerere na Karume, na Baraza la Mapinduzi likapelekewa hivyohivyo,” alisema na kuongeza: “Sasa ubishi wa hiyo hati ya kwanza kabisa ambayo wengi wanasema ipo Umoja wa Mataifa ilikopelekwa kuthibitisha nchi imebadili jina, hiyo ni ya nini? Ni ubishi wa bure tu.”
Sitta alisema kisheria kilichopitishwa na Bunge kinatambua yaliyomo katika hati hiyo na hali ndivyo ilivyo pia kwa Baraza la Mapinduzi.
Kwa takriban siku tatu, kamati kadhaa za Bunge zinazojadili Rasimu ya Katiba, zimekuwa na mgongano juu ya hati za muungano na uhalali wa saini za Nyerere na Msekwa.
Kanuni kutenguliwa - Alisema pia, Bunge la Katiba itabidi kubadili kanuni na ratiba yake katika kikao cha leo.
Sitta alisema kwa utaratibu uliokuwapo, leo kamati ndio zilipaswa kuanza kuwasilisha taarifa zake, lakini imeonekana haiwezekani.
“Ni kamati moja tu Namba 5, kati ya kamati 12 ndio ambayo ilikuwa imekamilisha kujadili na kupiga kura walau Sura ya Kwanza tu ya Rasimu, hivyo kwa hali ilivyo lazima tupitie upya kanuni zetu,” alisema Sitta.
“Tuliweka siku moja kwa ajili ya uandishi na kuandika ripoti, lakini haiwezekani, imebidi tuongeze siku nyingine moja ili wajumbe waweze kuipitia tena taarifa ya kamati ambayo itasomwa bungeni, vinginevyo itasababisha ubishi,” alisema.
Alisema marekebisho yote ya kanuni, yatafanyika leo bungeni na baadaye ndio itatolewa Ratiba ya Bunge katika siku zijazo.
Hata hivyo, alisema katika ratiba hiyo, kutakuwa na mapumziko ya Bunge Aprili 7, kupisha maadhimisho ya Siku ya Karume, baadaye Ijumaa Kuu, Sherehe za Pasaka na pia maadhimisho ya Sokoine na Muungano.
Chanzo - Mwananchi
Share on Google Plus

0 comments: