
“Tangu uhuru, taarifa ya CAG
inawasilishwa katika mkutano wa Bunge wa Aprili kila mwaka. Kwa hali ya
sasa, Rais atakaa na taarifa hiyo kwa zaidi ya miezi miwili akisubiri
Bunge kukutana.”PICHA|MAKTABA
Siku chache
baada ya Rais Jakaya Kikwete kupokea taarifa kutoka kwa Mdhibiti na
Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, utata wa kisheria
umegubika suala hilo kutokana na ukweli kuwa ibara ya 143 (4) ya Katiba
inataka Rais aiwasilishe bungeni taarifa hiyo ndani ya siku saba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe alisema jana kuwa suala hilo lina madhara katika utendaji wa Serikali.
“Kuna
madhara makubwa katika mzunguko wa uwajibikaji, kwani ni rahisi Serikali
kuichezea taarifa ya CAG kabla haijawa ya umma. CAG anakagua fedha za
Serikali kwa niaba ya wananchi kupitia Bunge. Hivyo ni lazima Bunge la
Katiba lipishe Bunge la Muungano ili kupokea taarifa ya CAG,” alisema
Zitto.
Aliongeza:
“Tangu uhuru, taarifa ya CAG inawasilishwa katika mkutano wa Bunge wa
Aprili kila mwaka. Kwa hali ya sasa, Rais atakaa na taarifa hiyo kwa
zaidi ya miezi miwili akisubiri Bunge kukutana.”
Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema siku hizo saba ni baada ya Bunge kuanza.
“Hakuna
utata wowote hapo, ukisoma vizuri kifungu hicho kinasema, Rais
atamuagiza waziri anayehusika kupeleka taarifa hiyo bungeni siku saba
baada ya Bunge kuanza, siyo siku aliyokabidhiwa. Kitu muhimu hapo ni
pale kikao cha Bunge kinapoanza bila kujali kinaanza lini,” alisema
Balozi Sefue.
“Katika hali ya kawaida, Bunge la Bajeti lilipaswa kuanza Aprili 8. Bunge la Katiba linahitaji pesa kutoka kwenye bajeti. Sioni namna Bunge la Katiba kuendelea kwa sasa. Itabidi liahirishwe mpaka Agosti,” alisema.
Suala la
kuahirisha vikao vya Bunge la Katiba kupisha Bunge la Bajeti lilielezwa
na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyesema atamshauri Rais Kikwete
kuangalia uwezekano huo.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge, Thomas Kashilila akizungumzia uwezekano huo, alisema Bunge hilo litasubiri ratiba ya shughuli za Bunge la Katiba.
Dk Kashilila alisema Kamati ya Uongozi wa Bunge la Katiba inatarajiwa kutoa ratiba ya shughuli zake kuelekea Bunge la Bajeti.
“Inapofika
Juni, Serikali inatakiwa kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya matumizi yake,
kwa hiyo mpango uliopo ni kuhakikisha kabla ya Juni 30, Bunge la Bajeti
liwe limeanza kazi zake,” alisema.
Chanzo - Mwananchi
0 comments: