Je, unajua kuwa unaweza kuupata mtandao wa kijamii wa Facebook kwa
gharama ndogo kabisa kwenye simu yako ya mkononi au pengine hata bila ya
gharama yoyote ukitumia teknolojia mpya iliyopewa jina la Facebook
'Zero'?
Kwa kuwa upatikanaji na utumiaji wa Intaneti kwenye mataifa
yanayoendelea ni changamoto kubwa kwa watoaji wa huduma hiyo, mitandao
ya Facebook na Google ambayo inaongoza kwa kuwa na watumiaji wengi
duniani, imekuja na suluhisho lao wenyewe kwa matumaini kwamba kutakuwa
na kiwango kikubwa zaidi cha watumiaji kwenye maeneo hayo ya dunia na
hivyo kuchochea ukuwaji.Kama ilivyo, kwa Google Zero, Facebook Zero nayo ni huduma ya kupokea taarifa za maneno tu bila ya picha na ambazo ni bure kwa watumiaji wake. Huduma hiyo inayopatikana kwenye kiungo cha 0.facebook.com inatafautiana kidogo na ile inayopatikana kwenye m.facebook.com ambayo kwa hakika ni kwa ajili ya watumiaji wa simu za mikononi pia.
Kwa mujibu wa msemaji wa Facebook, Brandee Barker, huduma hiyo "huondosha kiwango chochote cha taarifa ambazo huchukua nafasi kubwa kama vile picha". Nambari 0 imetumika kumaanisha kuwa aina hii ya huduma inaingizwa kwenye kiwango cha sifuri katika kampuni za simu za mkononi, na hivyo aina maalum za taarifa haziingizwi kwenye malipo ya mwezi au ya kifurushi.
Hivyo, mtumiaji anaweza kutumia mtandao wa intaneti kwa zile kurasa ambazo zimeingizwa kwenye orodha hiyo ya 0 kama huu wa 0.facebook.com, lakini tu kwa sharti la kuwa kwenye nchi ambayo inaruhusu huduma hiyo na simu yenye mfumo wa WAP.
DW Kiswahili kwenye Facebook Zero

Ndani ya kipindi cha miezi 18 tu tangu kuanzishwa kwake, watumiaji waliongezeka kwa asilimia 114 barani humo, na kufikia Disemba 2011, watumiaji wa Facebook barani Afrika walikuwa zaidi ya milioni 37.
Ukiichukulia takwimu hii kieneo na kinchi, utakuta kuwa nchini Nigeria peke yake, idadi ya watumiaji Facebook ilichupa hadi asilimia 154, Ghana asilimia 85 na Kenya kwa asilimia 50.
Ukiwa nawe na simu yako ya mkononi na unataka kuwa mchangiaji wa moja kwa moja kwenye matangazo yetu ya Idhaa ya Kiswahili ya DW kupitia Facebook, basi ingia kwenye 0.facebook.com halafu itafute DW Kiswahili. Kwa urahisi wa fedha na wakati, utaweza kuungana nasi moja kwa moja na kuchangia maoni yako kupitia ukurasa wetu wa Facebook.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Google/Facebook
0 comments: