Baada ya kushushiwa kipigo, bondia Japhet Kaseba amesema jambo lililompa faraja ni kutopigwa kwa Knock Out (KO) na Thomas Mashali katika pambano lao la kuwania ubingwa wa UBO Afrika lililofanyika kwenye ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es Salaam juzi.
Majaji wote watatu, Pembe Ndava, Robert Amos na Omary Yazidu walimpa ushindi Mashali wa pointi 97-94.
Kaseba alisema anaheshimu matokeo ya majaji kwani
wao ndiyo waamuzi wa mwisho na kueleza kuwa angejutia zaidi kama
angepigwa kwa KO, lakini kwa pointi bondia yoyote anaweza kupewa
ushindi.
Alisema licha ya kupigwa, hakuna cha ajabu
alichokifanya mpinzani wake kwenye pambano hilo ila raundi nne za mwanzo
ndizo zilimpa ushindi Mashali.
“Nilichelewa kufungua na kushambulia raundi nne za
mwanzo nikidhani namvutia muda mpinzani wangu ili achoke nami nimalize
mchezo, lakini ikawa ndivyo sivyo, mahesabu tu ndiyo yalikataa hakuna
kingine, najuta kwa nini nilimuachia acheze raundi za mwanzo,” alisema
Kaseba.
Katika pambano hilo la uzani wa light heavy,
Kaseba alianza vizuri raundi ya kwanza na dakika ya pili aliachia konde
la mkono wa kulia lililompata sawia Mashali na kumpeleka chini ingawa
alikuwa mwepesi kunyanyuka na kuendelea na mchezo kabla ya mwamuzi wa
pambano, Anthony Lutha kumhesabia.
Mashali alizinduka raundi ya pili hadi ya tano na
alicheza kwa kushambulia hali iliyosababisha mpinzani wake kujihami kwa
kukumbatia, kitendo kilichomfanya azomewe na mashabiki wa Mashali
waliojitokeza kwa wingi.
Raundi ya saba, nane na ya tisa, Kaseba
alibadilisha mchezo na kushambulia hivyo kumpa wakati mgumu mpinzani
wake ambaye katika raundi hizo alitumia muda mwingi kujihami.
“Kaseba alikuwa anaongea sana. Aliahidiwa gari
kama angenipiga hivyo zawadi hiyo imeota mbawa. Tangu mwanzo nilisema
Kaseba hana uwezo wa kunipiga akabisha sasa naamini amekubali kiwango
chake bado,” alitamba Mashali dakika chache baada ya kuvikwa mkanda wa
UBO Afrika.
Mashali alisema baada ya kipigo hicho hivi sasa
anajipanga ‘kumnyamazisha’ Karama Nyilawila ambaye atapigana naye Mei
Mosi jijini Dar es Salaam kuwania ubingwa wa dunia wa UBO.
Kaseba ana rekodi ya kushinda mapambano 5 (3 kwa
KO) amepigwa mara 4 (3 kwa KO) hajawahi kutoka sare tangu 2000
alipoingia kwenye ngumi za kulipwa.
Wakati Mashali ameshinda mapambano 10 ( 5 kwa KO),
amepigwa mara 2 zote kwa KO na kutoka sare mara moja tangu 2009
alipoingia kwenye ngumi za kulipwa.
0 comments: