JAMANI TUSIACHE SIASA ITUCHAGUE MFUMO WETU WA ELIMU

 
Kwa muda mrefu sekta ya elimu nchini imepitia mabadiliko mengi, pia kuzua hoja na maswali mengi yakiwamo ya siasa kuachwa itawale mfumo wa utoaji elimu katika nchi yetu.
Hali kadhalika, sekta hii imekutana na changamoto lukuki, zikiwamo malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakieleza kwamba elimu yetu inashuka kwa kiwango cha kutisha.
Hadi sasa zimetolewa sababu nyingi za kuporomoka kwa kiwango hiki cha elimu katika Tanzania katika miaka ya karibuni ambazo zinahusisha pande mbalimbali. Pande hizo ni pamoja na walimu, wanafunzi, wazazi au walezi, mazingira ya kujifunzia na kufundishia ambayo ni pamoja na madarasa, maabara, vitabu, ukosefu wa motisha hasa kwa walimu, utoro wa wanafunzi, mimba na kadhalika.
Ikumbukwe kuwa katika miaka ya karibuni ukiwamo mwaka jana, tumeshuhudia kushindwa vibaya kwa wanafunzi wetu waliohitimu kidato cha nne.
Matokeo hayo mabaya yaliiduwaza, kuilazimisha Serikali kuyafuta, kutaka usahihishaji, upangaji matokeo ufanyike upya na yote yalifanyika.
Kutokana na hilo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa niaba ya Serikali aliunda tume maalumu ili kuchunguza na kubaini kilichotokea.
Miongoni mwa kazi za tume ile zilikuwa ni kuchunguza na kubaini upungufu wote uliotokea na kisha kupendekeza ni hatua gani zinafaa kuchukuliwa.
Hata hivyo, ripoti ya tume hiyo ambayo iliongozwa na Profesa Sifuni Mchome, Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haijatolewa hadharani.
Ripoti hiyo imekuwa hata hivyo ikinukuliwa na vyombo vya habari ikionyesha upungufu mwingi katika elimu nchini.
Hali ikiwa bado ni hivyo, wiki hii, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetangaza mfumo mpya wa kutoa matokeo ya kidato cha nne na sita ambao utaanzia na wahitimu wa kidato cha nne ambao wanaanza mitihani yao kesho.
Uamuzi huo ambao umetangazwa na Profesa Mchome tayari umezua maswali mengi kutoka kwa wadau wakihoji kama kweli unalenga katika kuinua au kuporomosha zaidi kiwango cha elimu.
Wengine wameukosoa mfumo huo kwamba umefanyika zaidi kisiasa, unalenga katika kuwafurahisha wakubwa, hauna uhalisia na mazingira halisi ya elimu katika nchi yetu.
Share on Google Plus

0 comments: