SERIKALI KUWAPA WAKULIMA MIEZI MITATU NI VICHEKESHO

 
Hivi karibuni, wakulima wa mahindi mkoani Rukwa walipasua jipu kwa kuilalamikia Serikali kuhusu kitendo chake cha kuwakopa mahindi yao tangu Julai mwaka huu na hadi sasa haijawalipa.
Wakulima hao walitoa kauli zao kupitia vyombo vya habari, ambapo walilalamika kwa sauti za kukata tamaa kwa Serikali yao na kusisitiza kwamba wamechoka kuvumilia.
Ilielezwa kwamba Serikali kupitia Wakala wa Hifadhi ya Chakula cha Taifa iliwakopa wakulima lukuki wa mkoa huo tangu Juni, huku ikiwaahidi kuwalipa mapema Agosti.
Wakulima wa mkoa huo wanaidai Serikali zaidi ya Sh6 bilioni na mpaka sasa haijataja ni siku gani wakulima hao watalipwa.
Hali kadhalika wakulima wa zao hilo mkoani Ruvuma nao wametoa ya moyoni wakiilalamikia Serikali kwamba iliwakopa mahindi tangu Juni hadi sasa haijawalipa.
Meneja wa Wakala wa Hifadhi ya Chakula cha Taifa mkoani Ruvuma, Morgan Mwaipyana alikiri kwamba wakulima kudai zaidi ya Sh5 bilioni za mahindi waliyoikopesha Serikali.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alisema Serikali ililazimika kuwakopa wakulima, baada ya mahindi yao kuwa mengi kuliko makisio ya manunuzi.
Alisema kwa miezi miwili waliweza kukusanya zaidi ya tani 55,000 za mahindi ya wakulima wakati malengo yalikuwa chini ya tani hizo.
Sawa, pamoja na mambo mengi ambayo wakulima wanailalamikia Serikali, lakini suala la Serikali kuwakopa wakulima mazao yao kwa muda mrefu halieleweki kabisa.
Je, ni nani ama mfanyakazi gani wa Serikali asiyetambua jasho la mkulima linavyotoka akiwa shambani mpaka anadiriki kuchelewesha fedha za mkulima?
Ni nani asiyejua jinsi wakulima wanavyodamka asubuhi mapema na kujiingiza kwenye udongo kwa siku nzima wakibugia vumbi ama tope, wakilowa mvua ama kupigwa na jua ili kupata mavuno?
Je, wafanyakazi wa Serikali wanaochelewesha fedha za wakulima hao wana nia gani kwa chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015?
Share on Google Plus

0 comments: