GAZETI LA MWANANCHI KURUDI ULINGONI KWA KISHINDO BAADA YA KUUFUNGIWA


Gazeti la Mwananchi leo limerudi tena mitaani baada ya Serikali kulifungia kwa wiki mbili. Kama wasomaji wetu na wananchi kwa jumla wanavyokumbuka, Serikali kupitia Idara ya Habari (Maelezo) ililifungia gazeti hili Septemba 27, 2013 kwa madai kwamba lilichapisha habari mbili tofauti ambazo ilidai zilikuwa za uchochezi na kwamba zilikuwa na lengo la kuwafanya wananchi waichukie pamoja na vyombo vyake vya ulinzi na usalama.
Sio nia yetu hapa kueleza kwa undani maudhui ya habari tulizozichapisha na Serikali kuzitumia kama nondo ya kulifungia kwa muda huo mrefu. Hata hivyo, yafaa angalau kwa muhtasari tu kuweka sawa kumbukumbu za hatua hiyo ya Serikali ambayo tunasema bila kutafuna maneno kwamba ilikuwa ya uonevu na ya kiwango cha juu cha matumizi mabaya ya madaraka.
Hata hivyo, huu hakika sio wakati wa kumtafuta mchawi, kwa maana ya kutaka kujua nani hasa serikalini alitoa amri ya kulifungia gazeti hili kwa sababu ambazo sisi tunaona hazikuwa na chembe ya mashiko. Tulishangazwa kuona amri hiyo ya Serikali ikitolewa wakati mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete akiwa nje ya nchi, tena akiwa katika majukumu mazito ambayo dunia nzima ilikuwa ikiyafuatilia kwa shauku na umakini mkubwa.
Kulifungia gazeti wakati huo hatuoni kama ilikuwa kwa masilahi ya taifa kwa sababu hatua hiyo iliichafua taswira ya nchi yetu na bila shaka Rais Kikwete alijikuta katika wakati mgumu kila alipoulizwa kuhusu hatua hiyo iliyochukuliwa na Serikali yake.
Ni habari zipi zilizolipeleka gazeti hili kifungoni? Habari ya kwanza ilikuwa juu ya waraka kuhusu mishahara mipya ya watumishi wa Serikali ambayo tuliithibitisha pasipo kuacha shaka yoyote kutoka katika vyanzo vyetu vya habari vya kuaminika katika mamlaka za juu serikalini.
Tuliuchukulia kama taarifa muhimu sana kwa watumishi wa Serikali na wananchi kwa jumla na hatukuona sababu ya Serikali kutaka wananchi wafichwe kuhusu kuwapo kwa mishahara mipya kwa watumishi wake.
Itakumbukwa kuwa, wiki chache kabla ya gazeti hili halijachapisha habari hiyo, lilikuwa pia limechapisha habari kuhusu mishahara mipya katika sekta binafsi kwa mujibu wa waraka wa Serikali uliotolewa na Wizara ya Kazi na Ajira. Swali linalojitokeza hapa ni hili: Inakuwaje mishahara mipya ya watumishi wa Serikali iwe siri na mishahara mipya kwa sekta binafsi iwe kinyume chake?
Tunaamini kwamba utamaduni wa Serikali kuficha habari na taarifa zenye manufaa kwa umma siyo utawala bora hata kidogo. Ni hivi majuzi tu Rais Kikwete alipomwagiwa sifa na Rais Barrack Obama kwa kutia saini mkataba wa uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi.
Habari ya pili iliyochapishwa Agosti 17 mwaka huu na kusababisha gazeti hili kufungiwa ilihusu Serikali kuimarisha ulinzi katika maeneo ya karibu na misikiti jijini Dar es Salaam jana yake kufuatia kuwapo tetesi kwamba waumini wa Kiislamu siku hiyo wangeandamana kupinga kitendo cha Jeshi la Polisi kumuweka mahabusu Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda. Baadhi ya waumini walikuwa wameonyesha kukasirishwa na kitendo cha polisi kumwondoa Sheikh Ponda katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi) na kumpeleka katika Gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam.
Habari hiyo yenye kichwa cha habari; ‘Waislamu wasali chini ya ulinzi mkali wa polisi’ ilichapishwa ikiwa na mmoja wa mbwa waliokuwa na polisi katika doria kutokana na hofu ya kuzuka vurugu baada ya Swala ya Ijumaa, Agosti 16. Habari hiyo ilisema Waislamu hawakuandamana na waliswali kwa amani na utulivu na kwamba polisi hao waliokuwa na mbwa, huku wengine wakitumia pikipiki kufanya doria walitanda katika mitaa mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ulinzi. Lakini kwa mshangao wetu, Serikali katika kujaribu kuhalalisha kulifungia gazeti hili ilitoa tafsiri ya uongo kwamba habari tuliyochapisha ilisema kwamba mbwa walipelekwa katika maeneo ya ibada, wakati habari hiyo haikuwa na kitu kama hicho. Serikali ilidai katika taarifa hiyo, kwamba lengo la habari hiyo lilikuwa kuichonganisha na waumini wa Kiislamu ili waichukie pamoja na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, kwani kwa Waislamu mbwa ni haramu na picha hiyo iliudhalilisha Uislamu. Taarifa hiyo potofu ya Serikali imetuthibitishia pasipo kuacha shaka kwamba haikuwa na nia njema na gazeti hili.
Hatua ya kulifungia gazeti hili kwa sababu za kufikirika imesababisha maumivu kwa watu wengi. Vijana (vendors) waliokuwa wakiuza na kusambaza gazeti hili pamoja na familia zinazowategemea wameumia. Waandishi wa kujitegemea wanaolipwa kutokana na habari wanazotuma gazetini wameumia pamoja na familia zao. Hivyo hivyo, watoa matangazo na wasomaji waliokuwa wakilitegemea gazeti hili kwa habari za uhakika nao pia wameumia. Hasara ambayo MCL imepata kutokana na hatua hiyo ya Serikali haitamkiki.
Pengine huu ni wakati mwafaka wa kuikumbusha Serikali kwamba, gazeti hili pamoja na mengine yanayochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), ni magazeti makini sana yenye waandishi wa habari wanaoheshimu maadili ya taaluma yao. Hatusemi kwamba hatuwezi kufanya makosa, kwani sisi ni binadamu.

Share on Google Plus

0 comments: