ORODHA YA SILAHA ZA SUMU SYRIA HUWENDA ZIKATOLEWA LEO

Rais Bashar al-Assad wa Syria amesisitiza utayarifu wa serikali yake kukabidhi silaha za kemikali za nchi hiyo, na wakati huo huo akatahadharisha kwamba zoezi la kuziharibu laweza kuchukua muda mrefu, na fedha nyingi.
Rais wa Syria Bashar al-Assad Rais wa Syria Bashar al-Assad
Hayo Rais Assad aliyasema katika mahojiano na televisheni ya kimarekani, Fox News ambayo yamefanyika wakati wanadiplomasia katika Umoja wa Mataifa wakijadili mswada wa azimio linaloweza kuidhinisha mpango wa Urusi na Marekani, kuhusu kuharibiwa kwa silaha za kemikali za Syria ambazo kulingana na sheria ya kimataifa zimepigwa marufuku.
Kuhusu zoezi la kuziharibu silaha hizo, Assad alisema litachukuwa muda na kugharimu pesa nyingi, na kuiwekea changamoto Marekani.
''Litagharimu pesa nyingi, takribani dola bilioni moja, na litakuwa hatari kwa mazingira. Kama serikali ya Marekani iko tayari kulipa fedha hizo, na kubeba jukumu la kuzipeleka kemikali za sumu nchini Marekani, basi ifanye hivyo.'' Amesema Assad.
Mhanga wa al-Qaida
Akionekana mwenye kujiamini, rais Bashar al-Assad alisisitiza kwamba Syria haighubikwi na vita vya wenyewe kwa wenyewe, bali ni mhanga wa makundi ya wapiganaji yenye kuungwa mkono na kundi la al-Qaida, ambao alisema wamejipenyeza ndani ya nchi yake.
Assad amedai asilimia 90 ya waasi ni washirika wa al-Qaida Assad amedai asilimia 90 ya waasi ni washirika wa al-Qaida
Alikiri lakini kuwa vuguvugu la mageuzi nchini mwake lilianzishwa na wanaharakati wasio na msimamo mkali wa kiislamu, na kudai kwamba kuanzia mwishoni mwa mwaka 2012, harakati hizo zilikuwa zimetekwa nyara na wanamgambo wenye itikadi kali ya kidini. Kulingana na maelezo yake, kwa sasa asilimia kati ya 80 na 90 ya wapiganaji wa upinzani ni washirika wa mtandao wa al-Qaida.
Aidha katika mahojiano hayo rais Assad alisema Syria itatekeleza ahadi ya kukabidhi silaha zake za kemikali kwa jumuiya ya kimataifa, licha ya kukanusha shutuma kwamba serikali yake iliamuru mashambulizi ya kutumia silaha hizo tarehe 21 Agosti, karibu na mji mkuu Damascus.
Bado hakuna muafaka wa kidiplomasia
Rais Assad akijibu mashambulizi kupitia vyombo vya habari, majadiliano ya kidiplomasia juu ya mswada wa azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu silaha hizo za kemikali za Syria bado hayajapata muafaka.
Juhudi za kidiplomasia zinaendelea katika Umoja wa Mataifa kuhusu silaha za Syria Juhudi za kidiplomasia zinaendelea katika Umoja wa Mataifa kuhusu silaha za Syria
Mpango wa Marekani na Urusi kuhusu silaha hizo utapata mtihani mkubwa Jumamosi wiki hii, ambao utakuwa mwisho wa muda wa wiki moja uliotolewa kwa Syria kutoa orodha kamili ya silaha zake na mahali zinakopatikana.
Katika mahojiano na televisheni ya Fox News, rais Assad alisema orodha hiyo anaweza kuitoa hata kesho, na Urusi imesema imehakikishiwa na serikali ya Damascus kwamba itatoa ushirikiano ipasavyo.
Marekani, Uingereza na Ufaransa zimetayarisha mswada wa azimio ambalo linaruhusu matumizi ya nguvu dhidi ya Syria ikiwa itakaidi kuzikabidhi silaha zake za kemikali, lakini mswada huo hautoi kitisho cha moja kwa moja cha mashambulizi, wala cha vikwazo.
Naye katibu mkuu wa shirika la kujihami la NATO, Anders Fogh Rasmussen, amesema leo kuwa anaamini ni muhimu juhudi za kidiplomasia kuhusu Syria ziendelee kusindikizwa na uwezekano wa mashambulizi ya kijeshi.
Nchini Syria kwenyewe hali imeendelea kuwa ya wasiwasi, baada ya kundi moja la waasi lenye mafungamano na al-Qaida kuukamata mji mmoja ulio kwenye mpaka baina ya Syria na Uturuki.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE
Share on Google Plus

0 comments: