MR. NICE AINGIA TENA KWENYE MGOGORO BAADA YA KUTEMWA NA GRANDPA RECORDS


Nguli wa muziki aina ya ‘Takeu’ Lucas Mkenda ameingia katika mzozo mzito na meneja wake mpya baada ya kutokukubaliana baadhi ya mambo aliyokuwa akishauriwa na lebo hiyo mpya.
Mr Nice ambaye kwa sasa anamilikiwa na lebo ya Candy&Candy Records  kwa muda wa mwezi mmoja na nusu sasa baada ya kutoka katika familia kubwa ya muziki ya GrandPa Recods, ameelezwa kuwa alikuwa na mtazamo tofauti kibiashara na kampuni hiyo hali iliyotishia kuvunjwa kwa mkataba wao.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya Candy&Candy Records, Joe Kariuki alisema kampuni na mwanamuziki huyo anayependwa nchini Kenya ilitokea kutofautiana katika baadhi ya mambo hasa ubora wa kazi.
“Mr Nice ni msanii anayependwa sana hasa Mombasa, lakini wiki chache zilizopita tulikuwa na mabishano kidogo hii ilitokana na mtazamo tofauti hasa ni kutokana na wimbo wake mpya wa ‘Akina Mama’ binafsi ule wimbo sikuupenda na nilimshauri kwamba ni vyema tungetumia wimbo mwingine, lakini aling’ang’ania.
“Wimbo ule tuliupiga katika vyombo vya habari kwa bahati mbaya haukufanya vizuri lakini nilimtahadharisha mapema.
“Kampuni inaweza kupata  hasara, lakini tumeamua kuendelea na mkataba kwani kwa sasa ameelewa na tunakwenda kama kampuni inavyotaka,” alisema Kariuki.
Kariuki anasema nyota huyo aliyewahi kutamba na wimbo wa ‘Fagilia’ bado kazi zake zinaendelea kupendwa sehemu mbalimbali nchini humo.
“Tukifika sehemu kama Malindi, Mombasa na maeneo mengine mwanamuziki huyu bado ni chaguo la watu wengi. Anafanya vizuri lakini bado kuna mengi yanayomtinga ila ‘akikaza buti’ hakika atarudi na kuwa kama zamani hata Tanzania atashika chati za juu,” alisema.
Alisema muziki wa Bongo Fleva ni muziki pendwa nchini humo ndiyo maana kampuni hiyo imeingia mkataba na wasanii wengi kutoka nchini Tanzania wakiwamo Four - D, Top C, Mr Nice na Baby Madaha.
Wakati Mr Nice anaingia katika mgogoro huu mpya, miezi michache iliyopita aliondolewa katika Kampuni kubwa ya muziki ya GrandPa Records inayofanya kazi na wasanii wakubwa kama DNA, Ng’ang’a wa Tusker Project Fame na wengine.
Mr. Nice alipigwa chini na kampuni hiyo ambayo tayari ilikuwa imeshampigisha hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kumwandalia ziara ya kumtambulisha nchi nzima kwa lengo la kumwongezea mashabiki, kumpa shoo ya kumtambulisha na kuachia wimbo mmoja aliofanya na DNA uitwao ‘Tafuta’.
Share on Google Plus

0 comments: