MAGEREZA IWE NI SEHEMU YAKUANZA MAISHA


Ni jambo la kawaida kabisa kwamba taarifa zozote kuhusu Magereza nchini mwetu hazitakosa kugusia  msongamano wa wafungwa. Hali mbaya ya magereza na matatizo  lukuki kutoka kwenye chombo hiki muhimu kimojawapo cha Mfumo wa Haki Jinai (criminal justice system) ya nchi hii.
Sasa hivi unaposoma makala haya, idadi ya wafungwa Magerezani ni 34,587 (18.09.13) ambao ni mfuriko wa wafungwa uliozidi   idadi inayostahili kuwamo ndani ya Magereza kwa idadi ya 5,080.
Hivi karibuni pia Jaji Mkuu Othmani Chande wakati akifungua mafunzo kwa mahakimu ya Haki za Binadamu alidokeza pia umuhimu wa uharakishaji wa kusikiliza kesi za mahabusi ili kupunguza msongamano ndani ya Magereza.  Suala la msongamano wa wafungwa katika magereza yetu ni ukiukwaji wa haki za binadamu, alisema Jaji Mkuu.  Je, tutatokaje hapo?
Hivi karibuni gazeti hili lilitoa makala  iliyobeba jina “Magereza zinapofanishwa na jehanamu” lilijaribu kuelezea hisia za watu kwa chombo chao hiki ambacho kinapaswa kuwa ni eneo la mafunzo bora ya urekebishwaji wa wafungwa badala yake. Kulingana na makala  hayo iliyoandikwa na Dismas Lyassa, kwa namna inavyoonekana, ni kwamba Magereza yametumika zaidi kuwaharibu wafungwa na matokeo yake ni kwamba wafungwa asilimia 25 ya wanaoachiliwa hurudi tena gerezani.
Ni bahati mbaya kwamba si wengi, pamoja na wanasiasa wenyewe  wanaojua nafasi ya Magereza katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao.  Fikiria tu uwezekano siku moja wafungwa 1600 walioko sasa hivi  Gereza la Ukonga wavunje gereza na kuingia mitaani, je, jiji la Dar es Salaam litakuwa na usalama? Kwa wale wenye kumbukumbu nzuri watakambuka mwaka 1978/9  Gereza la Ukonga, wafungwa walipovunja gereza  wakiongozwa na jambazi Nyau  walivyotesa jiji la Dar es Salaam.
Kazi kubwa ya Jeshi la Magereza ni urekebishaji wa tabia za wafungwa ili kuwawezesha kujiunga na jamii kama raia wema  mara baada ya kumaliza vifungo vyao.  Kwa maana nyingine, kazi ya Magereza ni kudhibiti urudiaji (recidivism) wa wafungwa Magerezani na hivyo kuwafanya raia wema kuishi bila bugudha.
Ebu fikiria tena kwa mfano ule ule wa Gereza la Ukonga; iwapo wafungwa hao watatoka  gerezani kama walivyoingia bila ya urekebishaji wowote.   Wakitoka gerezani watakuwa na  uwezekano wa kushawishi wenzao wasiokuwa na kazi wajiunge na vikundi vyao ni dhahiri kwa jinsi hiyo ungezeko la uhalifu litazidi na  Magereza yatafurika kama ilivyo sasa na pia usalama wa raia utakuwa  shakani. 
Tafiti zinaonyesha kwamba endapo mfungwa anaweza kugunduliwa vishawishi vinavyo msababisha kutenda kosa (criminogenic factors) uwezekano ni mkubwa kabisa akipata tiba ya urekebishaji inayolenga kwenye tatizo lake anaweza kuacha uhalifu na kuwa raia mwema. Urekebishaji huchukuliwa kama tiba ya hospitali na ni muhimu kubainisha kwa uhakika wa tatizo ili kutoa tiba sahihi inayohusika.
Hii ndiyo kazi ambayo Jeshi letu la Magereza inapaswa kufanya na si kazi ndogo kama inavyodhaniwa.  Inataka kwanza  kuwe na utashi wa kisiasa ili kuwe na mabadiliko ya kifikra, kuwekeza katika vitendea kazi na rasilimali watu wa kutoa hiyo taaluma ya urekebishaji. 
Dhana hii  ya urekebishaji wa wafungwa ni mpya baada ya kugundulika kwamba utaratibu uliopo wa uendeshaji wa Magereza hausadii  urekebishaji wa wafungwa.  Badala yake utaratibu tulio nao unaongeza uhalifu na husababisha msongamano ndani ya magereza  kama takwimu zetu zinavyoonyesha, urudiaji wa vifungo ni asilimia 25 na msongamano ni zaidi ya 5,080
Kama nilivyodokeza hapo juu, taaluma hii  bado ni mpya, na inajulikana kama Mkakati wa Urekebishaji wa Wafungwa kwa kuzingatia tishio la uhalifu alionao  (Offender Risk Management and Correctional Strategy).   Kwa nchi zilizoendelea kama Canada, nchi za Scandinavia, Uingereza, Malaysia, Singapore, Korea, Australia, New Zealand zilikwisha anza  utaratibu huu tangu mwanzoni mwa miaka ya 80.   Kwa upande wa Afrika baadhi ya nchi tayari zimekwisha anza  utaratibu huu ambazo ni  pamoja na Afrika ya Kusini, Namibia, Zambia, Mauritius, Kenya, Nigeria na Ghana.
CHANZO MWANANCHI
Share on Google Plus

0 comments: