JAJI FRANCIS MUTUNGI: SUBIRINI MUONE UTENDAJI WANGU....



 Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman akimpongeza Francis Mutungi baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Jaji wa Mahakama Kuu katika hafla iliyofanyika Ikulu, Juni 19,2012. Jaji Mutungi jana aliteuliwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Msajili mteule wa Vyama vya Siasa nchini,  Jaji Francis Mutungi amewataka Watanzania kutulia na kusubiri utendaji wake atakapokabidhiwa rasmi jukumu hilo jipya alilopewa na Rais Jakaya Kikwete.

Mutungi aliteuliwa kushika wadhifa wa msajili wa vyama vya siasa kuchukua nafasi ya John Tendwa ambaye amestaafu. Tendwa aliiongoza taasisi hiyo kwa miaka 13.
Mutungi alisema: “Ninafahamu nina majukumu mazito mbele yangu, lakini siwezi kusema chochote kwa kuwa sijakabidhiwa rasmi ofisi. Ninachotaka kusema ni kwamba nitakuwa mtumishi wa kila mmoja.”
Alikataa kusema kuwa akianza kuzungumza mambo mengi kwa sasa wakati hajaingia rasmi kazini haitakuwa na maana yoyote na badala yake ataonekana kuwa anawahisha mambo.
Jana katika Mahakama Kuu ya Dodoma, ilikuwa tabu kumpata kiongozi huyo hali iliyoonyesha huenda alikuwa katika maandalizi ya kuweka mafaili yake katika hali nzuri kabla ya kuwaaga watumishi wenzake na kwenda kuanza majukumu mapya.
Wasaidizi wake wa karibu hawakuwa tayari kuelezea alikuwa na kazi gani hasa, lakini walimwambia mwandishi kuwa Jaji alikuwa na majukumu mengi kiasi cha kukosa nafasi ya kuzungumza na mtu.
Hata hivyo, alipompigia simu msajili huyo licha ya kukataa kuzungumza mambo mengi kuhusu nafasi yake hiyo mpya, lakini alionekana kuwa na ushirikiano wa kutosha na kuwataka wananchi wasubiri kitambo ili akabidhiwe. Juzi akizungumza na gazeti hili, Tendwa alikataa kumshauri Mutungi na kusema kuwa anaamini atafanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu kama ambavyo miongozo inavyotaka.
“Mutungi atafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kama ataanza kubezwa na wanasiasa afahamu kuwa sasa ndiyo anafanya kazi sawasawa.
Mawakili wamlilia
Mawakili mbalimbali wameelezea kuridhishwa na uteuzi wa Jaji Mutungi kuwa msajili wa vyama  vya siasa, huku wakimmwagia sifa kuwa ni mtu sahihi katika wadhifa huo na kwamba ana uwezo.
Wakizungumza na Mwananchi jana kwa nyakati tofauti, mawakili hao walisema Jaji Mutungi anafaa katika nafasi hiyo kulingana na sifa yake ya ujaji na uzoefu wa kisheria na kwamba wana imani kuwa ataiongoza vyema ofisi hiyo.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society- TLS), Francis Stolla na mawakili Richard Rweyongeza na  Jerome Msemwa, walimzungumzia Jaji Mutungi.
Share on Google Plus

0 comments: