RANGI NYEUSI KATIKA BENDERA YA TANZANIA INAMAANISHA NINI KATIKA TAIFA LETU

KABLA ya Tanganyika kupata uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1961, wananchi walikuwa wamegawanywa kwenye matabaka matatu; tabaka la kwanza Wazungu, hili lilikuwa ndiyo tabaka la juu lililoonekana bora kuliko mengine, neno la Kiingereza lililotumika kwa kundi hili ni “White people.”
Tabaka la pili lilikuwa la Wahindi na Waarabu ambao walionekana kuwa ni bora kiasi na kwamba, angalau walikaribiana na tabaka la kwanza na kwa Kiingereza lilijulikana “Coloured.”

Tabaka la tatu lilikuwa la Waafrika weusi lililokuwa la wenyeji wa Afrika (wazawa), neno la utambulisho kwa Kiingereza kufuatana na rangi ya ngozi yao ni “Blacks.” Kundi hili la tatu lilionekana kuwa duni na lilikandamizwa kwa kila hali na kuporwa rasilimali zao na kutumikishwa na waporaji.

Harakati za kujikomboa na kumkomboa mtu huyu mweusi za Chama Cha Tanganyika African National Union (TANU), zilipoanzishwa Februari 5, 1954 zililenga kuwakomboa watu wa tabaka la tatu yaani wazawa, weusi.

Bendera ya TANU ilikuwa na rangi mbili tu za kijani na nyeusi zikiwa zinamaanisha nchi kwa rangi ya kijani na watu weusi waliwakilishwa na rangi nyeusi.

Tanganyika ilipopata uhuru wake, Desemba 1961 bendera ya TANU ilibadilishwa kidogo kwa kuongezewa rangi ya manjano na ikawa bendera ya Tanganyika.

Hata hivyo Aprili 26, 1964 Tanganyika ilipoungana na Zanzibar na kuunda Tanzania, bendera ya Muungano ilikuwa na rangi zote za bendera ya Tanganyika lakini ikaongezwa rangi ya bluu.

Rangi za manjano na bluu zilikuwa na maana zake. Manjano; utajiri wa nchi ikimaanisha kuwa nchi imejaliwa rasilimali za madini na rangi ya bluu ikiwa inaonyesha rangi ya bahari, maziwa na mito iliyosheheni rasilimali nyingi, licha ya maumbo-nchi yenyewe kuwa ni rasilimali tosha.

Rangi nyeusi ilibakia kuwakilisha watu weusi (wazawa) na kijani utambulisho wa rasilimali ardhi inayotumika kwa uzalishaji wa chakula.

Historia hii inaonyesha wazi kwamba, Tanzania ni nchi ya watu weusi tangu awali kabla ya ujio wa wageni kama siyo wavamizi na watu hao weusi, ndiyo walikuwa wanakandamizwa hadi wakaunda vyama vya kujikomboa.

Ukombozi uliolengwa na vyama hivyo ulikuwa ni kupata uhuru wa kisiasa na kiuchumi na ndiyo maana kauli mbiu ya kwanza ya TANU mwaka 1961, ilikuwa ni “Uhuru na Kazi.”

Hata hivyo ni jambo la kusikitisha sana hivi sasa kusikia mtu mweusi katika Tanzania yenye uhuru wa miaka 50, bado anabaguliwa kutokana na rangi yake.

Mtu mweusi anabaguliwa kiuchumi katika nchi yake na wageni. Hii maana yake ni kwamba, rangi nyeusi katika bendera ya taifa haina maana yoyote.

Leo hii, mtu mweusi anaogopa kutamka neno ‘uzawa’ kwa sababu ataambiwa anaanzisha hisia za ubaguzi. Hapa ipo haja ya kutafakari kauli iliyowahi kutolewa na Wakili, Nimrod Mkono, aliyehoji kwamba uhuru wa Tanzania ulikuwa na maana gani kama mtu mweusi hana uhuru wa kiuchumi?

Kimsingi ni kwamba, uhuru wa kiuchumi ambao jamii ingependa kuwa nao ni kama haupo. Kinachojulikana kwamba jamii imewaondoa wakoloni na kujitawala wenyewe kimeingiliwa na wingu zito la ubeberu mamboleo ukiwa umejivika sura ya uwekezaji.

Kama ilivyokuwa enzi za kusaini mikataba na Carl Peters, haiyumkini kwamba historia haijatufunza jambo lolote kutoka kwake na udanganyifu alioufanya kwa watawala alioingia nao mikataba hususani Chifu Mangungo.

Baadhi inaweza kuonekana kuwa Mangungo kwa wakati huo hakuwa amesoma na kupata elimu, lakini kwa hivi sasa mikataba hiyo ya uwekezaji inasainiwa na wasomi, tena ambao wanaelewa mikataba wanayoingia inamaanisha nini na ina maana gani kama siyo manufaa gani kwa wanajamii wanaowawakilisha.

Taswira inayojitokeza hapa ni kwamba, ubeberu mamboleo unaingia kupitia mikataba na ukibeba sura ya uwekezaji na uwekezaji huo umejikita kwenye rasilimali za nchi ambazo ni madini na nyingine za kuvuna juu ya ardhi na kubwa zaidi ni ardhi yenyewe.

Tuchukulie mfano wa Hoteli maarufu hapa nchini ya Kilimanjaro, ambayo kimsingi ilijengwa na Serikali na kuitwa jina hilo ikiwa na maana hakukuwepo na hoteli kubwa kama hiyo tena nchini na hivyo ukubwa wake kulinganishwa na mlima Kilimanjaro. Lakini kwa upande mwingine hoteli hiyo kuitwa hivyo, ilikuwa ni njia ya kuutangaza Mlima Kilimanjaro.

Hali hiyo ilimaanisha kuwa pindi wanapotokea watalii na kudadisi maana ya jina hilo, ilikuwa ni rahisi kuwapa tafsiri yake kwamba limetokana na mlima huo na hivyo kuhamasika kutembelea maeneo ulipo na hata kuutangaza wanaporudi kwaoIlianza taratibu kwamba, ilibadilishwa jina kwa kuitwa Kilimanjaro Kempiski katika dhana hiyo ya uwekezaji hivi sasa neno hoteli ya Kilimanjaro ni jina mfu na kutangaziwa kuwa hata majengo yaliyokuwa jirani na yaliyotumika miaka mingi kwa ajili ya kuutangaza na kusimamia shughuli za Mtanzania nayo yanaelekea kumezwa na kufanywa maegesho ya magari ya wawekezaji wanaokuja kutumbua kwenye hoteli hiyo.

Tukumbuke kwamba, nyoka wote wanakaa vichakani, lakini ‘mfalme wa kichaka’ ni chatu. Mtu mweusi ni ‘chatu’ katika kichaka chetu

bara la Afrika, ndiye mwenye bara lake na ndiye aliyepata mateso kuliko mtu wa rangi nyingine yoyote katika sayari hii.

Miaka zaidi ya 500 ya utumwa na miaka zaidi ya 100 ya ukoloni mkongwe Afrika inatosha kutufundisha somo kwamba, mtu mweusi hana swahiba wake nje ya bara hili. Utandawazi ni aina nyingine ya ukoloni mpya wa kiuchumi na hivi sasa ndiyo unashika kasi.

Kama hatukujifunza kutokana na historia na kusikia ya watu werevu kama Wakili Mkono, tutarajie vizazi vijavyo kurudi tena utumwani karne ijayo. Tujikumbushe maana ya rangi nyeusi kwenye bendera ya taifa.
Share on Google Plus

0 comments: