HIVI NDIVYO MAUAJI YALIVYOFANYIKA HUKO DARFUR KUFATIA KUUWA KWA WANAJESHI 7 WA TANZANIA

Imefahamika kuwa kuuawa kwa wanajeshi saba wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliokuwa kwenye operesheni za Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa (Unamid), katika Jimbo la Darfur nchini Sudan, kulitokana na shambulio la kushtukiza (Ambush), lililopangwa na waliowashambulia.


Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange, katika salama zake alizozitoa kwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Dk. Jakaya Kikwete na waalikwa mbalimbali waliokuwa wamefika kwenye hafla ya kuwaaga mashujaa hao.


Jenerali Mwamunyange alisema wanajeshi hao waliuawa wakati wakisafiri kutoka eneo la Khor Abeche kwenda Nyala wakisindikiza msafara wa waangalizi wa amani wa Umoja wa Mataifa (UN).

“Ilikuwa ni Julai 13, saa tatu asubuhi na walipokuwa wamesafiri umbali wa kilometa 25, walifika kwenye eneo lililokuwa na mteremko mkali na lenye utelezi kufuatia mvua kubwa iliyokuwa imenyesha. Ilibidi wapunguze mwendo wa magari yao ili yaende taratibu, kumbe ndiyo walikuwa wanaingia kwenye ‘ambush’ na kujikuta wakishambuliwa,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, ilibidi wapigane kwa weledi mkubwa kwa karibu saa mbili ili kujinasua toka kwenye ambush hiyo, hadi pale walipopata msaada kutoka kwa askari wenzao waliokuja kuwasaidia.

Alisema kutokana na juhudi za kupigana kwa weledi kwa lengo la kujinasua, ilibidi waasi wakimbie, lakini tayari wakiwa wameshaua mashujaa hao saba na kujeruhi wanajeshi wengine 14, kati yao akiwamo ofisa mmoja wa polisi.

HALI ILIVYOKUWA
Shughuli ya kuaga miili ya mashujaa hao saba, Sajini Shaibu Othman, Koplo Oswald Chaula, Koplo Mohamed Ally, Koplo Mohamed Chikilizo, Private Fortunatus Msofe, Private Rodney Ndunguru na Private Peter Werema, ilianza saa tatu asubuhi kwa kuwasili wageni mbalimbali, wakiwamo mawaziri, mabalozi wanaowakilisha nchi zao na maofisa wa UN, maofisa waandamizi wa serikali, wakuu wa majeshi wastaafu na wanadhimu wastaafu.

Pia walihudhuria majenerali wastaafu, majenerali walio kwenye utumishi, wafanyabiashara, akiwamo Dk. Reginald Mengi, familia za wafiwa na wananchi wa kada zote.

VIONGOZI WA KITAIFA WAWASILI
Majira ya saa nne asubuhi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi aliwasili, akifuatiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal aliyewasili saa 4:52.

KIKWETE AWASILI
Rais Jakaya Kikwete aliwasili saa 5:08 asubuhi na shughuli ya kuileta miili ya mashujaa kwenye viwanja hivyo vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga, jijini Dar es salaam ilifuata.

MIILI YAWASILI
Lilianza gari lenye namba 5914 JW 12 lililokuwa limebeba jeneza la Sajini Othman, ambalo lilingia majira ya saa tano na robo asubuhi.

Jeneza hilo lilishushwa na askari wanane wenye vyeo vya sajini wakisindikizwa na askari wawili na kisha kupeleka jeneza hilo, juu ya meza moja maalumu iliyokuwa imeandaliwa.

Hatimaye lilifuata gari namba 5980 JW12 lililokuwa na jeneza la mwili wa Koplo Chaula, lililoingia saa 5:19, kisha gari namba 5907 JW12 lililokuwa na mwili wa Koplo Chikilizo, lililoingia saa 5:23 na gari namba 5913 JW12 lililioingia saa 5: 27, likiwa na mwili wa koplo Ally.

Baadaye lilifuata gari namba 5912 JW12 lililoingia saa 5: 32, likiwa na mwili wa Private Msofe, kisha gari namba 5976 JW12 lililoingia saa 5:36, likiwa na mwili wa Private Ndunguru na mwisho gari namba 5906 JW 12, likiwa na mwili wa Private Werema.

AMIRI JESHI AONGOZA
Rais Kikwete aliongoza waomboleza wote kuaga miili hiyo mnamo saa 5:47 pale alipopita mbele ya majeneza yaliyokuwa yamefunikwa kwa bendera ya taifa na kisha akamalizia kwa kuwapa mkono wa pole familia za wafiwa.

Baadaye Makamu wa Rais, Dk. Bilal alifuata akiwaongoza viongozi mbalimbali waliokuwa kwenye turubai kuu, wakiwamo mawaziri, mabalozi, maofisa wa UN, maofisa waandamizi wa serikali, majenerali wastaafu na maofisa wakuu walioko jeshini.

RISALA ZA RAMBIRAMBI
Zilisomwa rambirambi zilizotumwa kwa mkuu wa majeshi kutoka sehemu mbalimbali, zikiwamo toka kwa mabalozi, maofisa wastaafu, wanajeshi wenzao walio Unamid-Sudan na Jumuiya wa Watanzania wanaoishi Sudan. Aidha, Jumuiya ya Watanzania waishio nchini Sudan walitoa Dola za Marekani 700 kama rambirambi na wanajeshi wenzao walitoa Dola 1,800 kwa marehemu wote.

UN YATOA NISHANI
Katika kutambua mchango wa wanajeshi hao, UN ilitoa medali kwa kila mwanajeshi aliyefariki ambazo kwa mujibu wa Msemaji wa shughuli hiyo ya jana, Kanali Dominick Mrope, zitafikishwa kwa wanaostahili, kwa mujibu wa taratibu za kijeshi.

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Ali Mohamed Shein, alituma rambirambi kwa mkuu wa majeshi na katika salamu zake zilizosomwa kwa niaba yake na Kamanda wa Kamandi ya Nchi Kavu, Meja Jenerali Mustapha Kijuu, alisikitikia mauaji yaliyofanywa dhidi ya mashujaa hao.

“Natoa salamu zangu kwako mkuu wa majeshi na kwa familia za wafiwa, kufuatia msiba huu mkubwa wa kitaifa. Naomba tuwe na subira na nawatakia nafuu ya haraka, majeruhi wote walioko hospitalini,” alisema.

JK ANENA
Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema kwamba atahakikisha anatumia ushawishi wake wote ili kuzishawishi mamlaka za UN na Umoja wa Afrika (AU) zinazosimamia operesheni za amani Darfur, ili ziweze kuruhusu vikosi vinavyoshiriki katika operesheni hizo, kuwa na silaha nzito kwa minajili ya kujilinda kwa mapigo mazito, pale zinaposhambuliwa.

“Nilisikitika sana pale nilipopata habari ya kuuawa kwa mashujaa wetu. Nilijiuliza kwamba, kwa nini watu wa Darfur wawaue wanajeshi wetu walioenda kuwasaidia wapate amani, waendeshe maisha yao katika hali ya utulivu. Ndiyo maana niliongea na Rais Omar al Bashir, ahakikishe wanawatafuta wahalifu hawa haraka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria,” alisema.

Hata hivyo, Rais aliwaasa Watanzania na wanajeshi kwa ujumla kutokatishwa tamaa na kilichotokea, bali wachukue kama changamoto ya kujiimarisha zaidi.

Aliwakumbusha Watanzania kuwa toka uhuru, Tanzania imekuwa na falsafa ya kusaidia mataifa mbalimbali kwa njia za kidplomasia na kivita, ili yapate amani kama ilivyofanyilka katika nchi za Msumbiji, Liberia, Sierra Leone, Eritrea, Lebanon, Sudan na sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Alisema tokea Tanzania ianze kuchangia wanajeshi wake kule Sudan, mwaka 2007, JWTZ imefanya kazi zake kwa weledi na umakini wa hali ya juu, kiasi
cha kuiletea nchi sifa kubwa.

Alisema ni muhimu kuelewa kuwa, sehemu yoyote palipo na mazingira ya kivita kama ilivyo huko Sudan tulipokubali kupeleka wanajeshi, uwezekano wa kupata majeruhi na hata vifo kama ilivyotokea kwa mashujaa hao saba upo na kwa hali hiyo akaasa kusonga mbele.

WANAKOELEKEA MASHUJAA
Miili ya mashujaa hao ilisafirishwa jana kwenda sehemu mbalimbali, kwa ajili ya mazishi.
Sajini Shaibu Othman amepelekwa Zanzibar; Koplo Oswald Chaula, Kilolo-Iringa; Koplo Mohamed Ally, Zanzibar; Koplo Mohamed Chikilizo, Kigoma; Private Fortunatus Msofe, Tanga; Private Rodney Ndunguru, Songea na Private Peter Werema, Tarime.

HALI ILIVYOKUWA
Mazingira ya viwanja vya wizara yaligubikwa na simanzi kubwa kwa muda wote, huku bendi ya JWTZ ikitumbuiza kwa mbali kwa nyimbo mbalimbali za kijeshi.


Majira ya saa 7:25 mchana, ndipo msafara wa magari yaliyobeba miili hiyo, uliondoka katika viwanja vya Upanga, ikiwa imetanguliwa na pikipiki ya trafiki na gari ndogo ya Polisi wa kijeshi (MP), yenye namba 3365 JW11.



Share on Google Plus

0 comments: