ROMBO KIMENUKA POLISI WAAMUA KUSIMAMIA MAZISHI BAADA YA VURUGU KUTOKEA MSIBANI

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Said Mwema
KATIKA hali isiyo ya kawaida Jeshi la Polisi wilayani Rombo,limelazimika kusimamia shughuli ya mazishi baada ya kundi la watu wanne kuzuia mwili wa marehemu Gaspar Evarist (18) aliyefariki kwa ajali ya pikipiki usizikwe shambani kwake kijiji cha Muriae, wilayani Rombo.
Mkuu wa Polisi wilayani hapa, Ralph Meela alisema kuwa vurugu hizo zilisababishwa na mama wa marehemu huyo na watoto wake wakitaka mwili huo usizikwe kwenye shamba la baba yake mzazi bali wakauzike sehemu nyingine.
Akifafanua zaidi Meela alisema chanzo cha mzozo huo ni baba wa marehemu kufariki miaka mingi iliyopita na hivyo waliokuwa wakizuia mwili huo walidhani kuwa endapo marehemu atazikwa hapo shamba hilo litakua la kwake na hivyo watakosa urithi.
Alisema katika vurugu hizo zilisababisha uharibifu wa mali, kwani wahusika walivunja msalaba wa jumuiya pamoja na kumzuia padre kuendesha ibada ambaye ndugu walimtishia na hivyo kuondoka kuepuka vurugu hizo.
Baada ya polisi kufika waliwakamata watuhumiwa na kisha kusimamia mazishi hayo.
Wakati huo huo mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la
Lewanga Kimario (23) mkazi wa kijiji cha Mrere Mashati wilayani Rombo amefariki dunia baada ya kujinyonga. Mkuu wa Polisi Wilaya ya Rombo,Ralph Meela amethibitisha kutokea kwa tukio hilo. Meela alisema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 25, mwaka huu majira ya saa 9:00 alasiri katika Kijiji cha Mrere Mashati.
Meela alisema kuwa mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa umening’inia juu ya paa la nyumba yake.
Aidha alisema kuwa chanzo cha kifo hicho bado hakijajulikana. Kwa mujibu wa baba mzazi wa marehemu, Thomas Kimario alisema kabla ya tukio marehemu alikua akisumbuliwa na malaria kali na hivyo inaweza ikawa ndio sababu ya kifo chake.
Share on Google Plus

0 comments: