DONGO LA SUMAYE KUHUSU AJIRA KWA VIJANA LAMKOROGA EDWARD LOWASSA

WAZIRI Mkuu Mstaafu wa Serikali ya awamu ya tatu, Frederick Sumaye, amesema kuwa katu kukosekana kwa ajira nchini kwa vijana si bomu linalosubiri kulipuka. Bila kumtaja jina kauli hiyo ya Sumaye ilionekana kumlenga Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye hata hivyo bomu alilokuwa akilizungumzia ni ajira. Jana akizungumza na vijana wa Kawe Jogging, Sumaye alisema kauli kama hiyo imekuwa ikiwafanya vijana wajione ni kundi lingine, huku akihoji hatua walizochukua watu
hao kumaliza tatizo hilo.Alisema kama vijana wataweza kutambua wajibu wao kwa Taifa lao, katu hawezi kukatishwa tamaa na viongozi wenye matumaini ya uongozi kwa kutaka kuwafanya ni daraja lao la kupandiaMbali na hilo, Sumaye pia alizungumzia tatizo la rushwa nchini, akiwaonya Watanzania kuwa macho na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakipita kwa kutoa rushwa ili wapate uongozi katika ngazi mbalimbali ikiwemo Serikali Kuu.“Katika hili la mapambano dhidi ya ufisadi sitanyamaza kwani kila ninapotoa kauli za kupinga kuna baadhi ya watu hulalamika eti ninawashambulia, ninapenda kujua je hapa nimetaja jina la mtu. Kubwa ili wewe usiitwe mwizi ni lazima uache wizi, lakini ukiendelea kuiba utaitwa mwizi tu.“Rushwa imekuwa ikisambaa katika jamii yetu ya Watanzania, leo imefika mahali hadi watu wazima wananunuliwa na watu kwa maslahi yao, hili hapana msikubali vijana kufanya hivyo wala kuwapokea watu wa aina hii, kwani hata wakipata uongozi daima huyanufaisha makundi yao yaliyowazunguka na wala si Mtanzania wa kawaida,” alisema Sumaye.Alisema katika kipindi cha miaka miwili ijayo, nchi itaingia katika uchaguzi ambapo kuna watu watajitokeza katika ngazi zote na kuanza kutoa rushwa ya kanga, vilemba, fedha na hata kofia ili mradi tu waweze kupata uongozi huku akiwataka Watanzania na vijana kutokuwa tayari kuwaunga mkono.“Ikiwa unanunua hata uongozi kwa kutoa fedha, vijana watambue kuwa huyo mtu hatoshi kwani kama mimi ninatosha nina haja gani ya kuhonga watu fedha ili wanichague?” alihoji Sumaye.Waziri Mkuu huyo Mstaafu aliwaasa vijana kuwa wazalendo na kukataa kila aina ya makundi ya watu ambao wamekuwa wakitaka kuvuruga amani ya nchi na watu wake kwa kuondoa misingi ya uzalendo iliyokuwepo.
Share on Google Plus

0 comments: