RAIS Paul Kagame wa Rwanda amemteua
Mtanzania, Profesa Silas Rwakabamba pichani kuwa Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo
katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika Jumatatu iliyopita.Kabla ya uteuzi huo, Profesa Rwakabamba
alikuwa......
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda. Ni mmoja wa mawaziri
wanaoingiza sura mpya katika Baraza la Rais Kagame ambalo amelifanyia
mabadiliko kwa kuunda wizara nyingine mpya. Sura nyingine mpya katika Baraza
hilo ambalo liliapishwa juzi Ikulu ya Rwanda ni pamoja na Seraphine Mukantabana
(Wakimbizi na Menejimenti ya Maafa) na Oda Gasinzigwa (Ofisi ya Waziri Mkuu-
Familia na Jinsia).
Akizungumza kwa simu na mwandishi wetu
jana, mdogo wa Profesa Rwakabamba, Timothy Rwamushaija anayeishi Dar es Salaam,
alisema ndugu yake alizaliwa katika Kijiji cha Bushagara, Wilaya ya Muleba
mkoani Kagera. Alisema Profesa Rwakabamba alikuwa Mtanzania aliyeamua kuchukua
uraia wa Rwanda na wote baba yao ni Mzee Titus Rwamushaija... “Huyu ni kaka
yangu wa tumbo moja na kwa kweli tumefurahi sana kwa mafanikio yake sisi kama
wanafamilia.”
Naibu Makamu Mkuu - Taaluma wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Profesa Makenya Maboko alisema Profesa
Rwakabamba alifanya kazi katika chuo hicho na aliondoka akiwa Mkuu wa Kitivo
cha Uhandisi.
“Aliondoka wakati Kagame alipoingia
madarakani na alikwenda kuongoza Taasisi ya Teknolojia ya Kigali (KIST) kabla
ya kwenda katika Chuo Kikuu cha Kigali,” alisema Profesa Maboko.
Msomi huyo alikwenda Rwanda mwaka 1997,
baada ya kuombwa na Rais Kagame ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya
wahadhiri kwenda Kigali kufungua chuo kikuu katika taifa lake baada ya
kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994. Profesa Rwakabamba alikuwa
Mkuu wa kwanza wa KIST na kukifanya kuwa miongoni mwa vyuo bora barani Afrika
kwa masuala ya teknolojia jambo lililomfurahisha Rais Kagame.
Baada ya mafanikio hayo, Rais Kagame
alimteua kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda, Butare ambako pia
alijizolea sifa baada ya kusimamia vyema ujenzi wa mabweni kwa wingi na
kiongozi huyo alimtunukia uraia wa nchi hiyo kama zawadi. Hata hivyo, Profesa
Rwakabamba atakuwa amelazimika kuukana uraia wa Tanzania kwa kuwa katiba ya
nchi hairuhusu uraia wa nchi mbili.
Profesa Rwakabamba alipata elimu ya
msingi huko Muleba na akajiunga na Shule ya Sekondari ya Ihungo.
Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu
cha Leeds, Uingereza na kupata Shahada ya Uhandisi mwaka 1971 na 1975 alipata
Shahada ya Uzamivu katika fani hiyohiyo. Alirejea Tanzania na kujiunga na Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam katika Kitivo cha Uhandisi ambacho kilikuwa kimeanza
mwaka huo.
Alipata nafasi mbalimbali katika muda
mfupi aliokuwa hapo hadi alipotunukiwa kuwa Profesa mwaka 1981.
Mwaka 1985, Profesa Rwakabamba
aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mwanzilishi wa Mafunzo katika Kituo cha Afrika cha
Uhandisi Ubunifu na Uzalishaji (ARCEDEM), kinachodhaminiwa na Umoja wa Mataifa
(UN) kilichopo Nigeria. Baada ya kazi hiyo, ndipo alipokwenda Kigali. Tangu
1975, Profesa Rwakabamba amekuwa mjumbe wa bodi mbalimbali kitaifa na kimataifa
ikiwa ni pamoja na kuwa Bodi ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja
wa Mataifa (Unesco) na pia Kiongozi Mwandamizi wa Muungano wa Vyuo vya
Kimataifa (IAUP).
0 comments: