Kwa muda mrefu sekta ya elimu nchini imepitia mabadiliko mengi, pia kuzua hoja na maswali mengi yakiwamo ya siasa kuachwa itawale mfumo wa utoaji elimu katika nchi yetu.
Hali kadhalika, sekta hii imekutana na changamoto
lukuki, zikiwamo malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali ambao wamekuwa
wakieleza kwamba elimu yetu inashuka kwa kiwango cha kutisha.
Hadi sasa zimetolewa sababu nyingi za kuporomoka
kwa kiwango hiki cha elimu katika Tanzania katika miaka ya karibuni
ambazo zinahusisha pande mbalimbali. Pande hizo ni pamoja na walimu,
wanafunzi, wazazi au walezi, mazingira ya kujifunzia na kufundishia
ambayo ni pamoja na madarasa, maabara, vitabu, ukosefu wa motisha hasa
kwa walimu, utoro wa wanafunzi, mimba na kadhalika.
Ikumbukwe kuwa katika miaka ya karibuni ukiwamo
mwaka jana, tumeshuhudia kushindwa vibaya kwa wanafunzi wetu waliohitimu
kidato cha nne.
Matokeo hayo mabaya yaliiduwaza, kuilazimisha
Serikali kuyafuta, kutaka usahihishaji, upangaji matokeo ufanyike upya
na yote yalifanyika.
Kutokana na hilo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa niaba ya Serikali aliunda tume maalumu ili kuchunguza na kubaini kilichotokea.
Miongoni mwa kazi za tume ile zilikuwa ni
kuchunguza na kubaini upungufu wote uliotokea na kisha kupendekeza ni
hatua gani zinafaa kuchukuliwa.
Hata hivyo, ripoti ya tume hiyo ambayo iliongozwa
na Profesa Sifuni Mchome, Katibu Mkuu wa sasa wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi haijatolewa hadharani.
Ripoti hiyo imekuwa hata hivyo ikinukuliwa na vyombo vya habari ikionyesha upungufu mwingi katika elimu nchini.
Hali ikiwa bado ni hivyo, wiki hii, Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetangaza mfumo mpya wa kutoa matokeo ya
kidato cha nne na sita ambao utaanzia na wahitimu wa kidato cha nne
ambao wanaanza mitihani yao kesho.
Uamuzi huo ambao umetangazwa na Profesa Mchome
tayari umezua maswali mengi kutoka kwa wadau wakihoji kama kweli
unalenga katika kuinua au kuporomosha zaidi kiwango cha elimu.
Wengine wameukosoa mfumo huo kwamba umefanyika
zaidi kisiasa, unalenga katika kuwafurahisha wakubwa, hauna uhalisia na
mazingira halisi ya elimu katika nchi yetu.
0 comments: