Hivi karibuni, wakulima wa mahindi mkoani Rukwa walipasua jipu kwa kuilalamikia Serikali kuhusu kitendo chake cha kuwakopa mahindi yao tangu Julai mwaka huu na hadi sasa haijawalipa.
Wakulima hao walitoa kauli zao kupitia vyombo vya
habari, ambapo walilalamika kwa sauti za kukata tamaa kwa Serikali yao
na kusisitiza kwamba wamechoka kuvumilia.
Ilielezwa kwamba Serikali kupitia Wakala wa
Hifadhi ya Chakula cha Taifa iliwakopa wakulima lukuki wa mkoa huo tangu
Juni, huku ikiwaahidi kuwalipa mapema Agosti.
Wakulima wa mkoa huo wanaidai Serikali zaidi ya Sh6 bilioni na mpaka sasa haijataja ni siku gani wakulima hao watalipwa.
Hali kadhalika wakulima wa zao hilo mkoani Ruvuma
nao wametoa ya moyoni wakiilalamikia Serikali kwamba iliwakopa mahindi
tangu Juni hadi sasa haijawalipa.
Meneja wa Wakala wa Hifadhi ya Chakula cha Taifa
mkoani Ruvuma, Morgan Mwaipyana alikiri kwamba wakulima kudai zaidi ya
Sh5 bilioni za mahindi waliyoikopesha Serikali.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu
alisema Serikali ililazimika kuwakopa wakulima, baada ya mahindi yao
kuwa mengi kuliko makisio ya manunuzi.
Alisema kwa miezi miwili waliweza kukusanya zaidi
ya tani 55,000 za mahindi ya wakulima wakati malengo yalikuwa chini ya
tani hizo.
Sawa, pamoja na mambo mengi ambayo wakulima
wanailalamikia Serikali, lakini suala la Serikali kuwakopa wakulima
mazao yao kwa muda mrefu halieleweki kabisa.
Je, ni nani ama mfanyakazi gani wa Serikali
asiyetambua jasho la mkulima linavyotoka akiwa shambani mpaka anadiriki
kuchelewesha fedha za mkulima?
Ni nani asiyejua jinsi wakulima wanavyodamka
asubuhi mapema na kujiingiza kwenye udongo kwa siku nzima wakibugia
vumbi ama tope, wakilowa mvua ama kupigwa na jua ili kupata mavuno?
Je, wafanyakazi wa Serikali wanaochelewesha fedha
za wakulima hao wana nia gani kwa chama tawala Chama Cha Mapinduzi
(CCM), katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015?
0 comments: