Kwa siku za karibuni limetokea wimbi kubwa la vijana wa Kitanzania kukimbilia nchi mbalimbali duniani ikiwamo Afrika Kusini kwa madai ya kusaka maisha bora.
Baadhi ya vijana hao wamekuwa wakikamatwa na hata
kurudishwa nchini baada ya kukosa uhalali kisheria wa kuendelea kuishi
katika nchi hizo.
Wengine kati yao wamejikuta matatani kwa
kuhusishwa na usafirishaji wa dawa za kulevya pamoja na maovu mengine
baada ya kuingia katika nchi hizo kwa njia halali na zisizo halali.
Kwa upande wa Afrika Kusini, baadhi ya vijana hao wemeamua kuhamishia shughuli zao za kibiashara nchini humo.
Balozi wa Tanzania nchini humo, Radhia Msuya
anasema vijana wengi wanadanganyika kwa kufikiri kuwa maisha katika nchi
hiyo ni rahisi na kuwa baada ya kufika huko mambo yatakuwa rahisi na
kinyume chake mambo huwawia magumu na baadhi yao kuhitaji msaada wa
kurudishwa nyumbani.
Vijana 200 kwa mwezi
Balozi Msuya anasema kila mwezi wastani wa vijana
200 hurudishwa nyumbani Tanzania kutoka nchini humo kutokana na sababu
mbalimbali wakiwamo wale walioingia katika nchi hiyo bila vibali.
‘’Huku siyo peponi, maisha bora yanafanyiwa kazi
kama ilivyo huko nyumbani. Kila mwezi tunarudisha nyumbani vijana 200
wanaokamatwa mitaani hapa wakiuza bidhaa ndogo ndogo huku wengi wao
wakiwa hawana vibali,’’ anasema Balozi Msuya.
Anasema shughuli ndogo ndogo za biashara
wanazofanya vijana hao kutoka Tanzania haziwawezeshi kumudu gharama
kubwa za maisha nchini humo na baadhi yao hudaiwa kujihusisha na vitendo
vya uhalifu, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha, balozi huyo anawataka vijana wasiamini kuwa majibu yote ya changamoto zote zinazowakabili yanapatikana serikalini.
Anasema baadhi ya majibu ya changamoto hizo yako mikononi mwao na utatuzi wake siyo lazima kukimbilia nchini humo.
Anasema ni kweli Afrika Kusini imepiga hatua
kubwa kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwamo maendeleo ya
kiuchumi, ingawa pia yapo matatizo mengi ambayo vijana hukumbana nayo
baada ya kufikiri kwamba kukimbilia nchini humo litakuwa ni suluhisho la
matatizo yote waliyoacha nyumbani.
0 comments: