Serikali imesema mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini wanapaswa kutambua kuwa, wanawajibika kuheshimu Mkataba wa Kimataifa wa Vienna unaoainisha taratibu za diplomasia.
Pia, inasema inajiandaa kumwandikia barua Balozi
wa China nchini, Lu Younqing kutokana na hatua yake ya kujihusisha na
mambo ya siasa.
Wiki iliyopita, Balozi Lu alijitokeza kwenye
mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika mkoani Shinyanga, huku akiwa
amevalia moja ya sare za chama hicho, hatua ambayo imezusha mjadala
miongoni mwa vyama vya siasa na wachunguzi wa mambo ya kidiplomasia.
Akizungumzia kitendo hicho jana, Naibu Waziri wa
Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim,
alisema Serikali inajiandaa kumwandikia barua ya kumkumbusha wajibu wake
na kwamba itafanya hivyo baada ya kukusanya taarifa zake.
Hata hivyo, Mahadhi alisema Tanzania na China
zitaendelea kuwa marafiki wanaoshirikiana kwenye nyanja mbalimbali kwa
shabaha ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.
“Hizi taarifa za balozi kuwa kwenye mkutano wa CCM
nami zimezisikia na kuziona kwenye vyombo vya habari, tunachokifanya
sasa wataalamu wetu wanaendelea kuzifanyia kazi, baadaye tutamwandikia
barua kumkumbusha wajibu wake,” alisema.
Alisema siyo vyema kwa mabalozi kushiriki mambo ya
kisiasa, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Mkataba wa Vienna
ambao ndiyo unaotoa mwongozo.
Pia, Mahadhi aliasa vyama vya siasa kutoachia
majukwaa yao yakitumiwa na wanadiplomasia, akieleza kuwa navyo
vinawajibika kuheshimu mkataba huo.
Alisema iwapo pande zote zitaheshimu mkataba huo, hakutakuwa na kurushiana lawama.
0 comments: