Wenyeviti wa vyama vya Upinzani,Freeman Mbowe wa Chadema(Kulia) na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF(wapili kulia)wakiagana na viongozi wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu jijini Dar es Salaam jana baada ya mazungumzo kuhusu kupinga Rais kusaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba. |
Wakati vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vikiendelea na shinikizo la kutaka Rais Jakaya Kikwete asitie saini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amemwomba mkuu huyo wa nchi auridhie ili kuepusha vurugu ambazo zinaweza kujitokeza katika kikao kijacho cha Bunge.
Ameonya kuwa muswada huo ukirudi bungeni unaweza
kusababisha vurugu kubwa zaidi ya zile za mara ya kwanza kutokana na
tofauti kati ya wabunge wa CCM na wale wa vyama vya Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Chikawe alisema
kelele zinazopigwa na wapinzani hivi sasa hazisaidii kwa kuwa muswada
huo ulipitishwa baada ya taratibu zote kukamilika.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, atamshangaa
Rais Kikwete ikiwa atasikiliza kelele za wapinzani kwa sababu
walishirikishwa kupitia kamati na hata bungeni kabla ya kupitishwa
kwake.
“Nitamshangaa sana Rais Kikwete kama atashindwa
kusaini muswada huo kwa sababu ya kelele za wapinzani. Tuliwashirikisha
katika kila mchakato kabla na baada ya kuuwasilisha bungeni,” alisema
Chikawe.
Alisema kitendo cha wapinzani hao kujiunga pamoja
na kuanzisha kampeni za kuwahamasisha wananchi ili waukatae muswada
hakisaidii lolote, kwa sababu sheria zote zinatungwa bungeni na siyo
kwenye Viwanja vya Jangwani wala Ikulu.
Vyama vyampinga JK
Wakati Chikawe akisema hayo, viongozi wa Chadema,
CUF na NCCR-Mageuzi wameshikilia msimamo wao kwamba wataendelea kupinga
muswada huo uliopitishwa na Bunge, Septemba 6, mwaka huu.
Wakizungumza Dar es Salaam jana walipokutana na
Shura ya Maimamu ikiwa ni mwendelezo wao wa kukutana na asasi za kiraia,
viongozi wakuu wa vyama hivyo, walisema kamwe kasi yao ya kutaka
kutosainiwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
haiwezi kupunguzwa kwa namna yoyote kwa kuwa wanatetea masilahi ya
Watanzania na siyo mtu binafsi.
Kauli yao imekuja siku moja baada ya Rais Kikwete
kusema kuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakisema uongo kuhusu mchakato
wa Katiba unavyokwenda.
Wanasiasa pia hao wamepinga matumizi ya kauli za
kibabe kwenye mchakato huo na kuonya kuwa nguvu ya dola haiwezi
kushindana na nguvu ya umma.
Mbali na hayo, wanasiasa hao walisisitiza kwamba
hawatapiga magoti kuomba Katiba Mpya, kwani ni ya Watanzania wote na si
mali ya wanasiasa, chama cha siasa wala wabunge.
CHNZO: MWANANCHI
CHNZO: MWANANCHI
0 comments: