KAMA ULIKUWA UJUI KUHUSU FIDIA YA BAGAMOYO HII HAPA

Rais Jakaya Kikwete ametangaza kile tunachoweza kukiita neema kwa wakazi wa Bagamoyo ambao watahamishwa kupisha ujenzi wa bandari inayokusudiwa kujengwa na Serikali ya China. Rais aliiagiza Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji (EPZA), kwamba iwajengee nyumba wananchi watakaohamishwa ili wasiyumbe kiuchumi.  Rais alitoa agizo hilo kwa Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dk Adelhem Meru wakati alipotembelea banda la mamlaka hiyo katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Sisi hatuna ugomvi na agizo hilo la Rais ambalo tunadhani alilitoa kwa nia njema tu. Tukitilia maanani maisha ya taabu yanayowasibu wananchi wanaohamishwa kutoka sehemu wanazoishi ili kupisha miradi ya Serikali, tutagundua kwamba fidia zinazotolewa kwa wananchi hao ni kidogo mno na hakika haziwezi kukidhi gharama za maisha mapya kwa wananchi hao, zikiwamo za ujenzi wa makazi.
Wasiwasi wetu unakuja pale tunaposhindwa kuelewa vigezo alivyotumia kuona kwamba wananchi watakaohamishwa kupisha ujenzi wa bandari hiyo wanastahili kujengewa nyumba, wakati wananchi wengi wilayani Bagamoyo tayari wamechukuliwa ardhi yao kupisha miradi ya uwekezaji inayosimamiwa na EPZA kwa niaba ya Serikali. Jambo la ajabu ni kwamba wengi wa wananchi hao sio tu kwamba hawakujengewa nyumba, pia hawajalipwa fidia hata senti moja tangu ardhi yao ichukuliwe na Serikali miaka mitano iliyopita.
Hapa tunazungumzia wananchi wa vitongoji vya Gongoni, Kibuba, Mchanga wa Kichwa, Changuruwe, Mkungarungo na vingine kadhaa katika Kijiji cha Zinga. Hapa hatujataja vitongoji vingine nje ya kijiji hicho kama Kiromo, Pande, Makondo na kadhalika. Zipo fununu kwamba wananchi waliolipwa ni wale walio katika vitongoji ambavyo baadhi ya wamiliki wa ardhi ni vigogo wenye ukwasi na ushawishi mkubwa serikalini.
Tunachotaka kusema hapa ni kwamba tunadhani Rais Kikwete hajui kuwapo kwa hali hiyo. Kwa jinsi tunavyomfahamu, angejua hali hiyo angemwagiza kiongozi huyo wa EPZA na wizara husika ziwalipe wananchi hao fidia haraka iwezekanavyo. Hoja yetu hapa ni kwamba Rais angehimiza utekelezaji wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya 1999 (Na 4 & 5 ya 1999) chini ya Kanuni ya 6 kuhusu madai ya fidia ya ardhi ya mwaka 2001.
Ni kashfa na aibu kubwa kwa Serikali kuwadhulumu wananchi wake mchana kweupe, tena kinyume na sheria hiyo ya Ardhi tuliyoinukuu hapo juu. Wananchi hao wamekuwa wakiahidiwa fidia tangu mwaka 2009. Sasa wanateseka, wanalia na kusaga meno. Hawana pa kusemea, ingawa sasa wanajipanga kwenda mahakamani. Ardhi hiyo sasa imepanda thamani kiasi cha kutisha, lakini siyo yao tena. Walikuwa wakiitegemea kwa kila kitu. Upole wao na utiifu wa sheria umewaponza, kwa maana kwamba pengine wangeandamana na kufanya vurugu kama tunavyoshuhudia wengine wakifanya katika sehemu kadhaa nchini, huenda Serikali ingekuwa imewalipa fidia ya ardhi yao.
Tunamshauri Rais Kikwete aingilie kati suala hilo la fidia kwa wananchi hao. Inaonekana kwamba wizara husika za Fedha, Biashara na Viwanda, Ardhi pamoja na ile ya Uwekezaji hazina ushirikiano na pengine ndiyo sababu hazina habari na kinachoendelea. Hivi tujiulize, Serikali inapata faida gani inapotengeneza mazingira ya wananchi kuwa na chuki dhidi yake?
Chanzo - Mwananchi
Share on Google Plus

0 comments: