Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda kunukuliwa bungeni akiwataka polisi kuwashughulikia
kwa kuwapiga watu wote wanaokaidi kutii sheria.
“…Nasema wapigwe tu, maana tumechoka sasa,” alisema Pinda alipojibu maswali ya papo hapo Alhamisi iliyopita.
Akisoma tamko hilo bungeni jana, Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alisema kuwa kifungu cha 18(B) na
18(C) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kinatoa uwezo kisheria wa kutumia
nguvu za kadiri hata ikibidi kiasi cha kusababisha madhara au kifo
katika mazingira ya kisheria.
Aliyataja mazingira hayo kuwa ni pamoja na kuokoa
uhai wa mtu mwingine, kuzuia madhara makubwa ya mwili yasitokee kwake au
kwa mtu mwingine na kumzuia mtu anayetenda tendo ovu la kubaka au
kunajisi mtoto au kufanya vitendo kinyume na maumbile.
Pia kumzuia mtu anayevunja nyumba usiku au
unyang’anyi wa kutumia silaha au kuchoma nyumba moto au kufanya kitendo
chochote kinachohatarisha uhai wa mtu au mali.
Alieleza kuwa Kifungu cha 18 na 18(A) cha Sheria
ya Adhabu Sura namba16 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002, kinampa haki mtu
yeyote akiwemo askari kujilinda, kumlinda mtu mwingine, kulinda mali
yake au mali ya mtu mwingine ikiwemo ya Serikali na taasisi zake, ambayo
iko chini ya uangalizi wake kisheria.
Kauli hiyo ya Serikali kuhusu mauaji ya raia
mikononi mwa polisi, ilitolewa ikiwa ni ufafanuzi wa jibu la swali la
nyongeza lililoulizwa bungeni Mei 28,2013 na Rashir Ally Abdalah
(Tumbe-CUF), ambapo Silima alisema mauaji yanayofanywa na askari polisi
ni mauaji ya kisheria.
Kutokana na kauli hiyo, Mbunge wa Wawi, Hamad
Rashi Mohammed aliomba mwongozo wa spika kupata ufafanuzi wa kauli hiyo,
na jana Silima kutoa kauli ya Serikali kujibu mwongozo huo.
“Ikumbukwe pia kuwa, kifungu cha 29 cha Sheria ya
Jeshi la Polisi na Polisi wasaidizi Sura322, pamoja na Kanuni za Kudumu
za Utendaji za Jeshi la Polisi Na274, vinampa haki ya kisheria askari
polisi kubeba na kutumia silaha za moto ikiwamo bunduki na mabomu katika
utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku..,”alisema Silima.
Alifafanua kwamba katika kutafsiri sheria, kanuni
na taratibu mbalimbali ikiwamo alizozitaja, mahakama katika nyakati
tofauti imetoa msimamo wa kisheria juu ya suala hilo.
Akitoa mfano alisema: “Mathalan katika kesi ya
Seif Mohamed Senzagala dhidi ya Jamhuri ya mwaka 1994 kama
ilivyonukuliwa na Tanzania Law Report ukurasa wa 122, ambapo mshitakiwa
(mwomba rufaa) alimjeruhi kwa panga mlalamikaji ambaye alimfuata
nyumbani kwake na kuanza kumshambulia.”
Alisema katika kesi hiyo,mahakama ya rufaa pamoja
na kuridhia uamuzi wa mahakama ya awali wa kumtia hatiani kwa kutumia
nguvu kupita kiasi, ilibainisha kuwa mshtakiwa hakustahili adhabu kwani
alitenda kosa lile wakati akijihami dhidi ya mashambulizi toka kwa
mlalamikaji.
“Kwa msingi huo, tarehe 28 Mei, 2013 wakati nikijibu swali Na
290, nilitumia maneno ‘mauaji yanayofanywa kisheria’ nikimaanisha mauaji
yanayotokea katika mazingira niliyoeleza..,”alisema Silima.
Hata hivyo alisema siyo nia ya Serikali
kuhalalisha vitendo vya matumizi mabaya ya silaha ambavyo vinaweza
kufanywa na askari wasio waadilifu.
Alibainisha kuwa Jeshi la Polisi litaendelea
kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kuheshimu haki za raia na
kutumia busara kutatua migogoro.
Hata hivyo, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni
imelaani kauli ya Serikali kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi
iliyoitoa jana na kueleza kuwa haikubaliani nayo kwa kuwa inatoa baraka
kwa polisi kuendeleza mauaji ya raia.
Akizungumza na mwandishi wetu baada ya kikao cha
bunge kuahirishwa, Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani wa kambi hiyo rasmi,
Vicent Nyerere alisema kauli hiyo ingekuwa na uthabiti kama askari
polisi wangekuwa waadilifu.
“Kauli ingekuwa thabiti kama polisi wangekuwa
waadilifu. kabla ya kutoa kauli hiyo, Serikali ilitakiwa kuchuja
miongoni mwa askari wa jeshi la polisi, wa ngazi zote na kuwaondoa wasio
waaadilifu ndipo wakatoa kauli hiyo wananchi wataielewa
Serikali,”alisema Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini(Chadema).
Kwa upande wake, Mbunge wa Ole, (CUF) Rajab
Mbarouk Mohammed akizungumzia kauli hiyo ya Serikali alisema kuwa majibu
ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima ni ya kisiasa.
Alisema kwamba kauli hiyo ni mwendelezo wa kauli
iliyotolewa Alhamisi iliyopita na Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akiwataka
pilisi kuwashughulikia kwa kuwapiga watu wote watakaokaidi kutii sheria.
“Hakuna mwenye haki ya kuua, kuua ni kuua tu.
Mahakama pekee ndiyo ina haki ya kuhukumu kifo baada ya kumtia hatiani
mshtakiwa husika. Lakini kuwa polisi wanafundishwa utii, siyo
kuua,”alisema Rajab.
Alifafanua kuwa kazi ya polisi ni kulinda raia na mali zao na kwamba kuruhusiwa kujihami haimaanishi kuua raia.
Nao Wabunge Aeshi Hilaly na Aly Keissy walisema ni
vizuri raia wakatii mamlaka iliyopo na kutekeleza utii wa sheria bila
shuruti.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu alisema: “Maoni yangu haki za watuhumiwa lazima ziheshimiwe.”
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, (TLS), Francis Stola
alisema hakuna sheria inayompa mamlaka askari polisi kutumia nguvu za
ziada ikiwemo kupiga raia pindi anapotekeleza majukumu yake,isipokuwa tu
anaweza kutumia nguvu kiasi iwapo raia anayekabiliana naye anaonyesha
vitendo vya kukaidi amri ama kuhatarisha usalama.
Mwananchi:
Stola ambaye alikuwa akitoa ufafanuzi wa kisheria
kuhusiana na kauli bungeni alisema kuwa kwa kufuata sheria polisi
haruhusiwi kupiga raia. “ Ukisoma sheria hakuna mahala utakuta kuna neno
limeandika piga…. Askari polisi anachoweza kufanya ni arrest(kamata) na
siyo vinginevyo, hana mamlaka kabisa ya kupiga raia”
Alisema sheria imetamka wazi kuwa kunapojitokeza
hali yoyote inayopaswa kdhibitiwa na vikosi vya ulinzi, nguvu inayopaswa
kutumika ni ile ya kawaida na kwamba kitendo cha kutumia risasi za moto
ama kupiga raia ni ukiukwaji wa sheria za nchi.
Alisema polisi anapaswa kutoa mwongozo kwa raia
kumwelekeza jambo la kufanya iwapo kunajitokeza hali ya
sintofahamu,lakini hapaswi kutumia nguvu kupita kiasi ikiwemo kuwapiga
raia
“ Sheria inasema wazi kwamba panapojitokeza hali
yoyote korofi, polisi wanatakiwa kutumia nguvu ya kawaida tu kukabiliana
na hali hiyo na wala siyo kutumia silaha za moto… silaha za moto
zinaweza kutumika tu iwapo kunajitokeza tukio ambalo linaweza
kuhatarisha usalama wa maisha ama mali isipotee” alisema
Kuhusu wananchi kufanya maandamano, rais huyo
alisema maandamano ni haki ya msingi ya kila raia,lakini yanafanyika
katika utaratibu maalumu. “ maandamano ni haki ya kila raia lakini
panapaswa kuwa na utaratibu maalumu…. Kama kunajitokeza maandamano
ambayo hayana utaratibu polisi wanapaswa kutumia reasonable force (nguvu
ya kawaida) kudhibiti maandamano hayo na wala siyo kutumia nguvu za
ziada.
0 comments: