RAIS Barack Obama wa Marekani ameanza rasmi ziara
yake mjini Berlin nchini Ujerumani, iliyoanzia katika Ikulu ya Rais
Joachim Gauck ambako alikaribishwa kwa heshima. Katika ziara hiyo Obama
amepangiwa pia kukutana na Kansela Angela Merkel na kuhutubia umma
katika lango la Brandenburg ambako anatarajiwa kuitolea mwito Jumuiya ya
Kimataifa kuongeza bidii katika kuzishughulikia changamoto za dunia.
Rais Barack Obama aliwasili katika Ikulu ya Rais Gauck kwa
mazungumzo, kwa gari aina ya Limousine iliyopachikwa jina la The Beast,
chini ya ulinzi mkali akisindikizwa na msafara wa pikipiki. Katika ziara
hiyo rasmi mjini Berlin, Rais Obama atatumia muda wa saa 25 na dakika 5
kukamilisha ziara yake.
Rais Obama aliwasili Juni 18, 2013 nchini Ujerumani na kulala katika
Hoteli mjini Berlin akitokea katika mkutano wa kundi la nchi tajiri
kiviwanda duniani G8 uliomalizika Jumanne huko Ireland Kaskazini.
Ikiwa ni takriban miaka 50 tangu rais wa zamani wa Marekani John F.
Kennedy alipotowa hotuba yake na kutangaza “Ich bin ein Berliner yaani
mimi ni mkaazi wa Berlin” na miaka 26 tangu Ronald Reagan kutoa mwito wa
kuvunjwa ukuta wa Berlin, Obama atasimama palepale katika lango la
kihistoria la Brandenburg kutangaza mipango ya kupunguzwa kwa theluthi
moja silaha za Kinuklia za wakati wa vita baridi.
Inaelezwa kwamba Rais Obama akiwa na mwenyeji wake Kansela Angela
Merkel Rais Obama akiwa na mwenyeji wake Kansela Angela Merkel. Rais
huyo wa Marekani pia atafanya mazungumzo na Kansela Angela Merkel ambaye
kawaida anamuheshimu sana katika uhusiano wao.Hata hivyo katika mkutano
na Merkel Obama atakuwa chini ya shinikizo kubwa la kumtaka aeleze juu
ya umbali iliofikia mipango ya kijaasusi ya Marekani ya shirika lake la
usalama wa taifa la NSA ambayo inatajwa imekuwa ikikusanya data kuanzia
za simu hadi mitandao ndani ya Marekani na katika nchi za nje.
Merkel ameshasema atahitaji uwazi kutoka kwa Obama na kuongeza kwamba
wajerumani wanahitaji kufahamu ikiwa mienendo yao katika mitandao
imekuwa ikifuatiliziwa na NSA. Aidha katika hotuba yake kwenye eneo hilo
la kihistoria Obama anategemewa kupendekeza hatua ya kupunguza silaha
za kivita za Nuklia, mpango huo utazihitaji Marekani na Urusi kila mmoja
kupunguza kiasi silaha 1000 za Nuklia, huku pia akiiomba , Ulaya
kupunguza silaha zake za Kinuklia.
Hata hivyo haijawa wazi ikiwa rais wa Urusi Vladmir Putin ambaye
amekuwa na majadiliano makali na Obama nchini Ireland ya Kaskazini siku
ya Jumatatu, atakubaliana na mpango huo wa Obama. Awali itakumbukwa
Urusi ilitaka pafanyike mabadiliko katika mfumo wa ulinzi wa makombora
kabla kuiwafiki agenda hiyo ya Nuklia.
Polisi wamemiminika katika lango la Brandenburg atakakohutubia Obama
Polisi wamemiminika katika lango la Brandenburg atakakohutubia Obama.
Halikadhalika Obama ataweka wazi nia yake ya kuhudhuria mkutano wa
kilele kuhusu usalama wa Nuklia utakaofanyika The Hague mwaka ujao
pamoja na kutangaza kuandaa mkutano wake juu ya suala hilo mwaka 2016
ambao ni mwaka wake wa miwhso madarakani. Hotuba yake hiyo itakayotuwama
zaidi katika suala la Nuklia inalenga kuhakikisha kwamba suala la
kupambana na uenezaji silaha za Nuklia linabakia kuwa agenda yake muhimu
katika sera zake za Nje. Marekani inamiliki kiasi silaha 20 za kivita
za Nuklia ambazo bado zimewekwa Ujerumani.
Wakati wa kuanguka ukuta wa Berlin mwaka 1989 nchi hiyo ya Marekani
ilikuwa na kiasi silaha 200 za Nuklia za kivita ndani ya Ujerumani. Rais
Obama bado anapendwa na wajerumani, kwa mujibu wa utafiti wa maoni
uliofanywa wiki hii na gazeti la die Zeit unaonyesha asilimia 60 ya
wajerumani wameridhika na jinsi anavyoongoza.
-DW
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: