RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya
Mrisho Kikwete, Juni 20, 2013, amekutana na kufanya mazungumzo na
wajumbe wa Bodi ya Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA)
Ikulu, mjini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Rais Kikwete ameishukuru benki hiyo kwa kuendelea
kuunga mkono jitihada za.......
maendeleo ya Tanzania kwa misaada mbali mbali
ambayo imekuwa inatolewa na Benki hiyo kwa Tanzania.
BADEA imekuwa inaunga mkono shughuli za maendeleo ya Tanzania tokea
mwaka 1975 ilipofungua shughuli zake nchini na tokea wakati huo imetoa
kiasi cha dola milioni 175 hasa katika maeneo ya elimu, miundombinu ya
barabara na maji.
Katika mazungumzo hayo, ujumbe huo wa BADEA ukiongozwa na Mwenyekiti
wa Bodi ya Benki hiyo, Abdelaziz Khelef umemweleza Rais Kikwete uamuzi
wa Benki hiyo kusaidia mradi wa maji wa Mwanga-Same katika Mkoa wa
Kilimanjaro na pia kuangalia uwezekano wa kusaidia miradi ya kusambaza
umeme vijijini.
Wiki hii, Serikali ya Tanzania ilitiliana saini mkataba na Benki hiyo
ambako BADEA itagharimia mradi wa kusambaza maji katika maeneo ya
Mugango, Kiabakari na Butiama mkoani Mara, ujenzi wa Barabara ya Wete –
Chakechake, Kisiwani Pemba na kutoa msaada wa kiufundi kwa Kituo cha
Hesabu cha Pan African kilichoko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aidha, Rais kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa
kampuni ya kimataifa ya Marekani, General Electric ukiongozwa na John
Rice, Makamu Mwenyekiti wa kampuni hiyo katika mazungumzo yaliyofanyika
Ikulu, Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, kampuni hiyo imemweleza Rais Kikwete kuhusu
dhamira yake ya kuwekeza katika uchumi wa Tanzania kwa nia ya kuunga
mkono Visheni ya Maendeleo ya 2025.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: