KIKWETE AMCHENJIA WARIOBA KWAKURIDHIA MABADIRIKO YA KATIBA KUTAKA UWEPO MUUNDO WA SERIKALI MBILI

 
RAIS Jakaya Kikwete amemgeuka Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kwa kuridhia azimio la Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutaka uwepo muundo wa serikali mbili.
Rais Kikwete ambaye juzi aliongoza kikao cha Kamati Kuu (CC), mjini Dodoma, aliridhia azimio hilo, huku akijua fika kuwa ndiye aliyemruhusu Jaji Warioba kuingiza kipengele hicho kwenye rasimu wakati alipoifikisha mbele yake kabla ya kuitoa hadharani.
Kutoka na hali hiyo, Kamati Kuu imewataka wanachama wao wote kupitia mabaraza ya CCM kuhakikisha wanakubaliana na msimamo wa chama wa kupinga muundo wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa
na tume ya Jaji Warioba.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho kutoka Zanzibar, waliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa Kamati Kuu imepitisha azimio la kutaka mabaraza ya Katiba ya chama hicho yajadili na kuridhia msimamo wa kuwa na serikali mbili.
Kamati Kuu ya CCM imekuja na mapendekezo ya namna ya kurekebisha kasoro kubwa za Muungano ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikilalamikiwa na Wazanzibari.
Vyanzo vyetu vya habari vilisema kuwa baadhi ya wajumbe wa CC kutoka Zanzibar walimshambulia Jaji Warioba kwa jinsi alivyoingiza suala la serikali tatu katika rasimu huku akiujua fika msimamo wa CCM.
Hata katika mkutano wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulhaman Kinana na wabunge wa chama hicho uliofanyika mjini Dodoma, umesisitiza suala la serikali mbili tu.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika mjini Dodoma, zilisema kuwa wabunge nao walichambua kasoro nyingi za rasimu hiyo, kubwa kuhusu muundo wa muungano na mipaka yake.
“Kwenye mkutano wetu jana, tulikubaliana na msimamo wa Kamati Kuu wa serikali mbili na ndio ujumbe tunaupeleka kwa wananchi mikoani,” alisema mbunge mmoja alipozungumza na gazeti hili.
Mbali ya rasimu ya Katiba, Kamati Kuu ya CCM ilimshangaa Jaji Warioba kwa kupitisha sifa za wagombea urais na wabunge ambazo zinaweza kuleta mkanganyiko mkubwa siku za baadaye.
Katika mapendekezo ya rasimu kuhusu sifa za mtu kuwania ubunge, moja ya pendekezo hilo linasema kuwa, ikiwa “mtu huyo aliwahi kuwa mbunge kwa vipindi vitatu vya miaka mitano mfululizo, anapoteza sifa ya kuwa Mbunge.”
Katika sifa za kuwa rais, inasema, “ili uwe rais, lazima uwe na sifa za kuwa mbunge. “Hivyo kama umemaliza muda wa kuwa mbunge, maana yake hutakuwa na sifa za kuwania urais kwa vile huna sifa ya kuwa mbunge. Huu ni mkanganyiko mkubwa sana,” alisema mmoja wa wajumbe wa CC.
Share on Google Plus

0 comments: