.
Na Anna Nkinda – Singapore
Watoto waliotengwa na jamii kutokana na tabia ya kutokuwa na maadili
mazuri (watukutu) kama watapewa nafasi ya kupata mafunzo ya kutosha
ya dini, elimu ya darasani na kuonyeshwa msingi mzuri wa maisha
wanaweza kubadilika na kuwa watoto wema.Hayo yamesemwa leo na Mama Sahnim Sokaimi ambaye ni mkuu wa kituo cha
kurekebisha tabia za watoto wa kike watukutu cha PERTAPIS kilichoko
nchini Singapore wakati akiongea na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
alipo.......
tembelea kituo hicho.
Alisema kuwa chuo hicho kinawapokea watoto wa kike kuanzia umri wa
miaka 12 hadi 21 ambao mahakama imewakuta na makosa mbalimbali ikiwa ni
pamoja na uvutaji wa sigara chini ya miaka 18, utumiaji wa madawa ya
kulevya na kufanya biashara ya kuuza mwili (sexual activities).
“Tuliamua kuanzisha kituo hiki baada ya kuona kuwa kuna tatizo kubwa la
kuharibikiwa kwa watoto ikiwa ni pamoja na utumiaji wa madawa ya
kulevya lakini baada ya watoto hawa kuwapa misingi mizuri ya malezi na
maisha wameweza kubadilika na kuwa wasichana wema wanaofuata dini”,
alisema Mama Sokaimi.
Aliendelea kusema kuwa wasichana hao wamehukumiwa na mahakama kifungo
cha miezi sita hadi miaka mitatu kutokana na makosa mbalimbali
waliyoyafanya na wakiwa katika kituo hicho wanapata mafunzo ambapo baada
ya kumaliza kutumikia adhabu ya makosa yao wanakuwa wamebadilika
kitabia na kurudi kulelewa na familia zao.
Alimalizia kwa kusema kuwa wazazi wanatakiwa kuchangia gharama za
watoto wao kupata mafunzo kituoni hapo kiasi cha dola za Singapore 250
lakini wazazi wengi hawafanyi hivyo jambo ambalo linasababisha kituo
kukabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha na hivyo kuomba msaada kutoka kwa
wadau mbalimbali.
Kwa upande wake mama Kikwete aliwapongeza wafanyakazi wa kituo hicho
kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kurekebisha tabia za watoto wa kike
ambazo hazikubaliki na jamii na kuwafanya kuwa wasichana na wamama
wazuri ambao wanafanya kazi mbalimbali za kujitegemea kimaisha.
Mama Kikwete alisema kuwa jukumu la kuwalea na kurekebisha tabia za
watoto ni la jamii nzima na kuwaomba wafanyakazi wa kituo hicho kuja
nchini ili nao wajifunze na kuona ni jinsi gani wanaweza kushirikiana
kwa pamoja kuwasaidia watoto wenye matatizo kama hayo.
Aidha mama Kikwete pia alitumia taaluma yake ya ualimu na kutumia muda
mfupi aliokutana na wasichana hao na kuwafundisha somo la kiingereza kwa
kuwaelekeza umoja na wingi wa baadhi ya vitu.
Kituo hicho chenye jumla ya wasichana 54 kilianzisha mwaka 1990 kinatoa
mafunzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu ya Sekondari na msingi kwa
wale ambao walikatisha masomo yao, ufundi wa kujitegemea, mapishi, stadi
za maisha, utengenezaji wa nywele, ushonaji wa nguo na mafunzo ya
kiroho.
Mama Kikwete ameambatana na mumewe rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Singapore kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: