Hotuba ya
Kambi ya Upinzani kuhusu Makadirio na Mapato na Matumizi ya Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, jana ilisababisha shughuli za
Bunge kusitishwa kwa muda, kwa kile kilichoelezwa kuwa imejaa maneno ya
uchochezi. Hotuba
hiyo iliyokuwa ikisomwa na Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo, Mbunge wa Mbeya
Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi, maarufu kama Mr. Sugu, ilisitishwa
mara baada ya Mbunge wa..... Mbozi Mashariki (CCM), Erasto Zambi, kuomba
mwongozo.
Zambi alisema kuwa katika ukurasa wa kwanza hadi wa 14 wa hotuba hiyo
kumejaa maneno ya uchochezi yanayosema kuwa serikali ya CCM inafanya
vitendo vya kiharamia vya kuwateka na..... kuwatesa waandishi wa habari kwa
kuwango’a meno, macho na kuwatoa kucha.
Zambi
aliomba mwongozo kupitia kifungu cha 68 (1) na Kanuni ya Bunge ya 6
(a), akisema kuwa Mbunge aliyekuwa akiendelea kutoa hotuba anatoa maneno
ya uchochezi ambayo hayawezi kuvumiliwa.
Baada ya Zambi kuomba mwongozo huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda,
alisema analazimika kuahirisha kikao hicho cha Bunge ili hotuba hiyo ya
kambi ya upinzani ikafanyiwe marekebisho kabla ya kusomwa tena.
“Sisi wenyewe juzi hapa tumepitisha azimio la kukataa mambo ya uchochezi
humu, sasa nasitisha kikao cha Bunge hadi jioni ili kamati ya kanuni ya
Bunge ikae na kufanyia marekebisho hotuba hii,” alisema Makinda.
Kwenye hotuba yake, Sugu alisema Tanzania imeingia rasmi katika orodha
ya fedheha ya mataifa ambayo taaluma ya habari ni taaluma ya hatari kwa
wale wote wanaoitumikia kama sehemu ya wajibu wao kwa taifa na kama
ajira kwao.
Katika hotuba yake, Sugu alisema kuna ushahidi kwamba serikali ya CCM na
Jeshi la Polisi wamekuwa wakihusika na kuwaua na kuwaumiza waandishi wa
habari wanaoandika habari zisizowapendeza viongozi wa serikali na
Jeshi la Polisi.
Alisema miezi sita baada ya kuuawa kwa Daudi Mwangosi, mwandishi
mwingine mwandamizi, Absalom Kibanda, alitekwa nyara na kuteswa vibaya
nje ya nyumba yake.
Sugu alisema Kibanda alitekwa na kuteswa baada ya nyendo zake
kufuatiliwa na polisi na watu wengine wanaodhaniwa kuwa ni watumishi wa
Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS).
Alisema badala ya kuchukua hatua za dhati na kuwachukulia hatua
waliohusika na tukio hilo la kigaidi, Jeshi la Polisi likishirikiana na
Idara ya Usalama wa Taifa, maofisa wandamizi katika Ofisi ya Rais Ikulu
na viongozi wandamizi wa CCM walianzisha kampeni ya kuichafua Chadema.
Sugu alisema CCM iliamua kuanza kumsingizia Mkurugenzi wa Usalama wa
chama hicho, Wilfred Lwakatare kwa madai ya kuhusika na ugaidi kutokana
ushahidi wa kutunga tunga.
Sugu alisema kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kulinda Waandishi wa
Habari Ulimwenguni (CPJ), iliyotolewa mwaka huu 2013, kwa mara ya kwanza
tangu kuanzishwa kwa CPJ mwaka 1992, Tanzania imeingizwa kwenye orodha
ya nchi 20 ambazo ni hatari kwa waandishi wa habari kufanya kazi zao
kutokana na hatari ya kuuawa kwa mwaka 2012.
Alisema kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania ilishikilia nafasi ya saba
ulimwenguni kati ya nchi 20 zinazoongoza kwa kuhatarisha maisha ya
waandishi wa habari. Mbunge huyo alisema kwa mujibu wa taarifa ya CPJ,
tishio kubwa kwa waandishi wa habari duniani ni kuuawa kwa kutekwa na
kuteswa au kutishiwa maisha.
Aidha, alidai kwamba serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ni
washiriki wakubwa wa mauaji ya waandishi wa habari na kwa mujibu wa
takwimu za CPJ, kati ya waandishi waliouawa mwaka 2012, karibu asilimia
20 waliuawa ama na maafisa wa serikali au na majeshi yake.
Alisema karibu idadi hiyo hiyo ya waandishi wa habari waliuawa kwa
sababu ya kufuatilia taarifa za kiuchunguzi na za hatari na taarifa hiyo
inaonyesha kwamba hadi kufikia Aprili 2013, waandishi wa habari wapatao
30 tayari wamekwishauawa ulimwenguni wakati wakitimiza wajibu wao
wakati mwaka 2012 waandishi wa habari 103 waliuawa ulimwenguni kote.
Baada ya Bunge kurejea jioni, Spika Makinda alitoa maelekezo kwa Kambi
ya Upinzani kutosoma ukurasa wa kwanza hadi wa 14, lakini Sugu alisoma
hotuba yake kuanzia ukurasa wa 12 na kuzimiwa kipaza sauti.
Baada ya kuimaliza, Zambi alisimama kuomba mwongozo wa Spika akitaka
aelezwe ni jambo gani lilisababisha maelekezo ya Spika ya kubadilisha
hotuba hiyo yasitekelezwe huku akilalamikia hatua ya Sugu kuisoma bila
kufanyiwa marekebisho.
Hata hivyo, Spika alisema kuwa hotuba hiyo haitakuwa katika kumbukumbu za hansard.
DK. SLAA AJA JUU
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, amesema ikibidi Bunge
livunjike au wabunge wa chama hicho wafukuzwe bungeni, lakini hawako
tayari kuzibwa mdomo kuzungumzia masuala yanayohusu maisha ya
Watanzania.
Amesema chama hicho hakitakubali wabunge wake wapangiwe mambo ya
kuzungumza kwa kutegemea busara za Spika au Naibu Spika, bali
wataangalia na kufuata maelekezo ya kanuni za Bunge, akisema ndiyo
msingi wa uendeshaji wa chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi.
Akizungumza katika mikutano ya hadhara jana katika maeneo ya Ngalangala,
Basotu, wilayani Hanang na Haydom, wilayani Mbulu, kuhusiana na hotuba
ya Sugu kuahirisha Bunge, Dk. Slaa alisema wabunge wa chama hicho daima
wataendelea kuwasemea Watanzania wanyonge ndani na nje ya Bunge.
“Moja ni tukio lililotokea leo (jana) bungeni. Kwa wale mliofuatilia
mkutano wa Bunge mliona kilichotokea. Ninachotaka kumwambia Spika na
wasaidizi wake bungeni ni kwamba Bunge linaongozwa kwa kanuni za bunge,
si vinginevyo.
Uamuzi aliofanya wa kuagiza hotuba ya wabunge wetu ipelekwe kwenye
Kamati ya Maadili ya Bunge ni kinyume na kanuni ambazo ndizo msingi wa
utendaji kazi wa bunge. Hakuna sehemu yoyote katika kanuni inampatia
mamlaka Spika ya kupeleka hotuba ile kwenye kamati hiyo, ili waelekeze
nini kisemwe. Hakuna,” alisema Dk. Slaa.
Alisema kuwa baada ya mawasiliano ya viongozi wa juu wa chama hicho na
uongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, walikubaliana kuwa kwa sababu
hotuba hiyo haikuvunja kanuni yoyote ile ya Bunge, hawatakubali kuondoa
au kupunguza neno hata moja.
CHANZO: NIPASHE
0 comments: