POLISI MTWARA WAHUSISHWA NA VITENDO VYA UBAKAJI NA UPORAJI


Familia ya Mariam Abdllah,Mkazi wa mtaa wa Mtawike,kata ya Magomeni Mtwara,ikiwa chini ya baada ya nyumba yao kuteketezwa kwa moto na watu wasiojulikana katika ghasia zilizozuka ambapo baadhi ya wanachi wanapinga kusafirishwa kwa gesi asilia kutoka Mtwara kwenda Dar es salaam.
Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, limeingia katika kashfa ya matumizi makubwa ya nguvu kwa kufanya vitendo vya udhalilishaji na kuua raia kwa risasi. Katika maeneo mengi,  wananchi wamedai kuchomewa nyumba, kuibiwa mali, maduka kuchomwa moto, baadhi ya wanawake kubakwa na kuuwawa. Hadi sasa kuna utata mkubwa juu ya idadi ya watu waliofariki ama kuuawa katika vurugu hizo, huku kukiwa na taarifa za kukinzana kati ya Mkuu wa...... Mkoa wa Mtwara, Polisi na Hospitali ya Rufaa ya Ligula.
  Mkuu wa mkoa huo, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia, amethibitisha kutokea kifo cha mjamzito, Fatuma Mohamed, huku asijue chanzo chake, na kwamba hana taarifa za vifo vingine.
 
Naye Kamanda wa Polisi mkoani humo, Linus Sinzumwa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, watu wawili wamepoteza maisha katika ghasia hizo. Aliwataja kuwa pamoja na Fatuma, yumo pia Karim Shaibu (22), mkazi wa Chikongola, aliyefariki Mei 22, mwaka huu.
 
“Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, nina taarifa ya kifo cha mtu mmoja, mjamzito, mazingira ya kifo chake siwezi kuyaeleza,” alisema Simbakalia alipotakiwa kufafanua utata huo.
 
Lakini Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamed Kodi, alisema hadi sasa amepokea maiti mbili, na majeruhi 18 ambao hali zao zinaendelea vizuri.

MADAI YA MAUAJI
 
Hata hivyo, wananchi wamepinga vikali taarifa za serikali kwa madai kuwa zimepotosha ukweli, kwa kuwa wananchi waliojeruhiwa na kupoteza maisha ni wengi na wengine wameshazikwa. Katika kata ya Mikindani,  wananchi wamemtaja Mussa Mohamed mkazi wa mtaa wa Jangwani, kuwa ameuwawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wakiendesha doria ya nyumba kwa nyumba.
 
Said Kajuba, alisema aliyefariki ni ndugu yake na wakati anapigwa risasi, aliona na wametoa taarifa polisi pasipo kupata msaada. Katika eneo la Magomeni-Likombe karibu na kiwanda cha Olamu, wananchi wamedai kuna watu (hawakutaja idadi) waliouawa, ingawa hawakuwatambua kwa majina.

BIBI KIZEE ALILIA NYUMBA, WATOTO WAKE
 
Mkazi wa mtaa wa Mtawike, kata ya Magomeni, Mariam Abdalah, amedai kuchomewa nyumba na askari waliofika eneo hilo kwa ajili ya kuwakamata wahalifu.
 
Mariam alisema wanawe wawili walikimbia na hadi sasa hajui walipo. “Kama mnavyoona sina pa kuishi, nyumba imechomwa moto, ninalala nje, nilinunua chakula cha akiba kimeungua chote, wanangu wawili sijui walipo, nimewaona askari wa kike akiwasha kiberiti kuchoma nyumba yangu ya nyasi,” alidai.
 
 
NYUMBA KUCHOMWA MOTO
 
Mkazi wa mtaa wa Magomeni Tulivu, Magomba Abdalah, alidai nyumba sita za wananchi zimechomwa moto na kwamba hasira zao (wananchi) zilizidi baada ya polisi kufanya hujuma badala ya kuwalinda na kutuliza ghasia.
 
“Askari waliofanya vitendo hivi si wa Mtwara mjini wala hatuwajui, ni wageni wameletwa kukabiliana nasi.”
 
“Tunatarajia askari wawe walinzi wa raia ila wamechoma nyumba, wameiba mali, wametupiga sana, kwa hali hii ni ngumu kuona kuwa ni watu wema kwetu,” alisema.
 
Aidha, alisema kwa sasa kuna uhasama mkubwa kati ya polisi na wananchi kwa kuwa sehemu za biashara zinazodaiwa kuchomwa moto na askari wa jeshi hilo, zilikuwa kitega uchumi cha vijana wasiojua hatima yao.
 
 “Serikali inatupeleka wapi, kwenye mtaa wetu askari kachomewa nyumba, hakuwa na tatizo na mtu, ila hasira za wananchi zimetokana na polisi wageni kuchoma vibanda na maduka yao, hali si nyepesi kama inavyoonekana, askari wageni wataondoka hawa tunaobaki nao itakuwaje,” alihoji Magomba.
 
 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, ametembelea maeneo yalioathiriwa na vurugu hizo, ikiwamo ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), mahakama ya mwanzo Mikindani na nyumba za
askari polisi watatu.

DIWANI WA CCM AIUMBUA POLISI
 
Katika eneo la Mikindani, diwani wa kata ya Magengeni, Omary Nawatuwangu, alisema askari polisi wamehusika kuchoma nyumba za wananchi na kuharibu mali.
 
Kutokana na kauli hiyo, Nchimbi, `alimbana’ diwani huyo kwa maswali, akihoji uhakika wa kuwa polisi wamehusika na kwanini wananchi walifanya uharibifu wa mazingira ikiwamo kutaka kubomoa daraja.
 
Diwani huyo kupitia CCM, alisema akiwa nyumbani kwake, walifika polisi wakimuomba asaidiane nao kutoa magogo yaliyokuwa yamepagwa barabarani.
 Alisema, baada ya hapo aliwaona wakiwasha moto kwenye vibada vya biashara eneo la kituo cha mabasi cha Mikindani na kuchoma nyumba ya bibi mmoja anayeishi peke yake.
 
Nawatuwangu, alisema hadi kufikia jana, baadhi ya watu waliendelea kukaa misituni kutokana na hofu ya kupigwa ama kuuwawa kwa risasi, kwa kuwa polisi wanavunja
milango na kukamata wananchi waliopo majumbani.

MSIMAMO KUHUSU GESI
 
Baadhi ya wananchi wa tarafa ya Mikindani, Mawazo Mtonya, Mzee Issa Salum Nambanga, Fatuma Mfaume, Said Kajuba, walielezea ukosefu wa ajira kuwa miongoni mwa vyanzo vilivyochochea vurugu kwenye eneo hilo.
 
 “Kuna Bahari ila haturuhusiwi kuvua hadi uwe na nyavu kubwa, hatuna shughuli za kibiashara, kupatikana kwa gesi tuliona ni neema kwetu ila serikali inaleta siasa kwenye hili, hatutakubali tunataka gesi itunufaishe,” alisema Said Kajuba.
 
Alisema madai yao kwa serikali ni kuanza ujenzi wa viwanda mkoani humo, ili wananchi wapate ajira na kipato cha familia na si kusafirissa gesi hiyo kwenda Dar es Salaam kabla ya kuanza kwa ujenzi husika.
 
“Tunachokiona serikali inataka kutufanyia kiini macho, wanataka kujenga bomba la gesi kabla ya viwanda na uwekezaji wowote hapa kwetu, endapo gesi itasafirishwa kwa bomba uwekezaji mkubwa utakuwa Dar es Salaam nasi tutaendelea kuwa masikini,” alisema Nambanga.
 
Abidi Salum mkazi wa Mikindani, alisema hawana pingamizi na gesi hiyo kunufaisha Watanzania wote, lakini viwanda vya kuchakata gesi ni muhimu vikajengwa Mtwara na gesi safi isambazwe.
 
“Kama sisi tukihitaji gesi ya kutumia inafuatwa Dar es Salaam, kwanini wasije kuchukua huku, hatutaki isafirishwe kwa bomba, itakwenda nyingi,
wakishindwa watumie magari, nyaya au meli,” alisema Salum.
 
POLISI WANENA, MMOJA ABUBUJIKWA MACHOZI
 
Baadhi ya askari waliochomewa nyumba na mali kuharibiwa, walisema hali hiyo imewashtua na wamewatambua baadhi ya raia waliofanya vitendo
hivyo. Mmoja wao, Koplo Philemon, alibubujisha machozi mbele ya Nchimbi, wakati akielezea tukio la kuharibiwa na kuibiwa mali kwenye nyumba yake.
 
Hata hivyo, Nchimbi, alimtaka kuwa jasiri kwa kuwa askari anatakiwa kuwa jasiri muda wote. Katika nyumba wa Mwandishi wa TBC, Kassim Mikongolo, ambaye mke wake ni askari polisi, PC Fatuma Mohamed, ilielzwa kuwa wahusika wa uhalifu huo walifanya hivyo mara mbili na wametangaza kwa yeyote atakayemsaidia, watamdhuru kwa kumchomea nyumba.
 
“Nyumba yangu imechomwa mara mbili, awali tuliokoa baadhi ya vitu, tumeviweka nje, polisi walipoondoka, wahalifu wakarudi na kuiba kuku wote, nina baadhi ya vitu vya kuhamishia kwa ndugu lakini wanaogopa, wahalifu walitahadharisha watakaotusaidia, nyumba zao zitachomwa moto,”alisema. 
 
SIMBAKALIA NAYE…
 
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Simbakalia, alisema iwapo itabainika askari polisi wamehusika na vitendo vya kikatili vinavyolalamikiwa, watachukuliwa hatua.
 
“Zipo njia nyingi za ofisi za wakuu wa wilaya na mkoa kupokea taarifa za malalamiko, wanawake au wasichana waliobakwa waje kutupa taarifa, ikibainia hakuna askari atakayeachiwa kwani vitendo hivyo ni kinyume na maadili ya kazi zao,” alisema.
 
Alisema kwa sasa hali ya usalama imerejea na wanawahamasisha wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji.

WAANDISHI WA HABARI WANUSURIKA KIPIGO
 
Waandishi wa habari walinusurika kupigwa katika eneo la Mkanaledi, ambako kulikuwa na kundi la vijana waliodai (waandishi) hawaandiki ukweli na wanaipendelea serikali.
 
Kutokana na hali hiyo, waandishi hao walilazimika kukimbia, kila mtu akielekea upande wake na wengine kupoteana.
 
MCT YASISITIZA USALAMA WA WAANDISHI
 
Mapema katika mkutano na waandishi wa habari, Mkuu wa mkoa wa Mtwara alipouliza juu ya uwezekano wa kuwapatia ulinzi waandishi , alisema Katiba inasema ulinzi ni wajibu wa raia wote, hivyo wajilinde na kwamba jeshi la polisi halina polisi wa kulinda kila  mtu nyumbani kwake.
 
Wakati kiongozi huyu akitamka hivyo, tayari Baraza la Habari Tanzania(MCT) limeshatoa taarifa kwa vyombo vya habari likisisitiza pamoja na mambo mengine ombi kwa serikali ifanye kila linalowezekana kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa waandishi na raia wengine wote wa mkoa wa Mtwara.
 
Pia MCT limetoa rai kwa wamiliki wa vyombo vya habari na menejimenti zake kuchukua kila hatua za dharura kuhakikisha usalama wa waandishi wao huko Mtwara.
 
Lakini pia waepuke kufanya maamuzi ya aina yoyote yanayoweza kuhatarisha maisha ya waandishi wao walioko huko. Aidha waandishi wawe waangalifu kuhakikisha hawajiweki katika mazingira hatarishi.
 
 
CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

0 comments: