Machafuko
yamelipuka katika Manispaa ya Mtwara Mikindani baada ya wananchi wa mji
huo kuchoma moto ofisi za serikali na nyumba za viongozi wa serikali
takribani sita, ikiwamo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala
za Mikao na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia na inaripotiwa
kuwa mtu mmoja amekufa katika vurugu hizo na wengine kadhaa ku........jeruhiwa.
Wananchi
hao wamefanya uasi huo na uharibifu mkubwa wa mali kupinga uamuzi wa
serikali kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam kabla ya
kujua mikoa ya kusini itanufaika vipi.
Uchomaji huo ambao pia ulihusisha ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ulianza kutekelezwa jana kuanzia saa 5:00 asubuhi baada ya Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuwasilisha hotuba ya
bajeti ya mwaka 2013/2014 katika kikao cha........
Bunge mjini Dodoma.
Bunge mjini Dodoma.
Taarifa ambazo NIPASHE imezipata na kuthibitishwa na viongozi wa
serikali wa wilaya ya Mtwara, zilieleza kuwa ofisi za serikali za kata
za Majengeni, Mtonya na Changani zilichomwa moto.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa, alisema kuwa watu
91 walikamatwa kuhusiana na vurugu hizo ambazo zilijitokeza zaidi katika
maeneo ya Magomeni na Soko Kuu la Mtwara.
Alisema kuwa nyumba kadhaa za askari polisi mjini Mtwara zilivunjwa na
kwamba kutokana na vurugu hizo, abiria waliokuwa wanasafiri kwenda
Mtwara kutokea Dar es Salaam waliishia Lindi kuhofia usalama wao.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile, alisema ofisi ya CCM
Wilaya ya Mtwara, ofisi ya Mbunge wa Mtwara Mjini (CCM), Hasnain Murji,
na nyumba ya Waziri Ghasia zilichomwa moto.
Alisema wananchi hao pia walichoma jengo la Mahakama ya Mwanzo Mikindani
na kwamba hadi saa 11:40 jioni hali ilikuwa tete katika mji wa Mtwara
kutokana na wananchi kuendelea kufanya vurugu ambazo zilifuatana na
uharibifu wa mali.
Nyumba ya mtangazaji wa Shirika la Utangaza Tanzania (TBC), Kassim Mikongoro, ilichomwa moto.
Alisema dalili za kutokea machafuko hayo zilianza mapema jana asubuhi
kutokana na huduma mbalimbali ukiwamo usafiri wa magari, pikipiki na
maeneo ya kutolea huduma za afya kusitishwa, hali iliyozua wasiwasi
mkubwa kwa wananchi.
“Tangu asubuhi huduma za mama lishe, usafiri wa bodaboda, bajaji,
mabasi, hospitali na vituo vya mafuta vilivyopo mjini Mtwara hawakufanya
kazi kama serikali tukaanza kujipanga kwamba hapa kutakuwa na vurugu,”
alisema Ndile.
Alisema baadaye vurugu zilianza kulipuka na wananchi kuanza kuzichoma
moto ofisi nne za serikali za kata za Mtwara Mjini na ofisi ya CCM
wilaya na kufanya uharibifu wa mali za watu kadhaa.
Kabla ya RPC Sinzumwa kuelezea hali hiyo, DC Ndile alisema kutokana na
vurugu hizo hadi kufika sa 9:30 alasiri, watu zaidi 50 walikuwa
wamekamatwa na Jeshi la Polisi kuhusiana na ghasia hizo na kwamba hadi
saa 4:30 jioni mji wa Mtwara ulikuwa haujatulia kutokana na wananchi
kuendelea kufunga barabara kuu.
Mkuu huyo wa wilaya alisema madai ya wananchi hao ni kupinga gesi ya
Mtwara kusafirishwa kwenda Dar es Salaam kabla ya kujulishwa kama
watanufaika vipi na nishati hiyo.
Meya wa Manispaa ya Mtwara, Msharika, alisema hali ilikuwa tete na kwamba kila mkazi wa mji huo alijifungia nyumbani kwake.
“Unavyoongea na mimi hapa nimejifungia ndani na familia yangu hasa
ukizingatia sisi viongozi ni ‘wanted’ (tunatafutwa), mabomu yanaendelea
kupigwa kila eneo na vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kutekeleza
kazi yake.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Mohamed Sinani, alisema alipata taarifa za kuchomwa kwa ofisi ya CCM Wilaya ya Mtwara.
“Hivi sasa nipo Dar es Salaam, lakini nimepewa taarifa kwamba ofisi ya
CCM imechomwa moto, lakini sijafahamu sababu hasa za wananchi kufanya
tukio hilo,” alisema Sinani.
SHULE ZAFUNGWA
Taarifa zaidi ambazo NIPASHE ilizipata zilieleza kuwa kutokana na vurugu
hizo, shule za msingi za Shangani na Chikongola zilifungwa kwa muda na
wanafunzi waliruhusiwa kurejea kwao hadi hapo watakapotangaziwa tena.
Mwalimu Charles Makolo wa Shule ya Msingi Shangani, alisema
wamewarejesha wanafunzi majumbani kwao kwa siku mbili hadi hapo hali ya
usalama itakapotengamaa.
Mwalimu Joseph Kandeo wa Shule ya Msingi Chokongola, alisema waliwarejesha wanafunzi kwao hadi hapo watakapotangaziwa tena.
Taarifa zinaeleza kuwa dalili za kutokea machafuko hayo zilianza baada
ya kusitishwa ghafla kwa matangazo ya TBC katika mji wa Mtwara saa 2:00
wakati wananchi hao wakifuatilia mkutano wa Bunge.
Wananchi walianza vurugu hizo kwa kuchoma matairi barabara na mitaani
hali iliyolilazimu Jeshi la Polisi kupiga mabomu kuwatawanya, lakini
vurugu hizo zilisambaa katika maeneo mengi ya mji huo.
“Ona sasa hata matangazo ya bunge wamekata, wanamaanisha nini wakati
sisi tunahitaji kufahamu hatma yetu,” alisema Ali Hamis mfanyabiashara
wa Soko Kuu.
Hamis alidai kuwa kusitishwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya mkutano
wa Bunge ni njama za serikali ili wananchi wa mikoa ya kusini wasiweze
kusikiliza suala la gesi.
Hata hivyo, ilipofika saa 3:55 asubuhi matangazo ya Bunge ambayo yanarushwa na TBC kutoka mjini Dodoma yalirejea.
Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, vikao huanza saa 3:00 asubuhi kwa kipindi
cha maswali na majibu hadi saa 4:00 asubuhi. Hotuba na miswada mingine
ya serikali hufuata baada ya kipindi hicho kuanzia saa 4:00.
Jana hotuba ya Waziri wa Nishati na madini ilianza kusomwa takribani saa 4:20.
Ilipofika saa 6:00 mchana askari waliokuwa katika doria maeneo ya Soko
Kuu la Mtwara vijana walilizunguka huku wakiwazomea kwa kuwarushia
mawe.
Vurugu hizo ziliendelea kwa wananchi kufunga barabara kuu ya Mtwara-Dar
es Salaam kwa kuweka mawe na magogo katikati katika eneo la Mkanaledi na
baadaye polisi walifika eneo hilo na kufungua barabara hiyo.
Aidha, waandishi wa habari mkoani hapa walipata wakati mgumu kutekeleza
majukumu yao kutokana na wananchi madai kuwa baadhi ya wananchi walitaka
kuwadhuru kwa kuwatuhumu kuwa wanaandika taarifa kuegemea upande wa
serikali.
HALI YA USAFIRI
Machafuko hayo yalisababisha mji wa Mtwara kukumbwa na tatizo la usafiri
kutokana na vyombo vinavyotoa huduma ya usafiri kusitisha huduma.
Salum Juma, mwendesha boda boda mjini Mtwara, alisema kuwa alipokea
vitisho kutoka kwa wananchi wakimtaka kuacha kupakia abiria na kuwa
atakayekaidi atalazimisha pikipiki yake itachomwa moto.
UPORAJI
Diwani wa Kata ya Likombe, Mukhusin Komba, alisema wananchi walivamia
nyumba yake na kuvunja duka, kuiba vitanda vitatu na magodolo manne.
Meneja wa Posta tawi la Mtwara, Omari Kilimo, alisema kuwa toka asubuhi
hakukuwa na mteja aliyefika katika ofisi yake kwa ajili ya kupata
huduma.
HOSPITALI YA RUFAA LIGULA
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Ligula, Mohamed Kodi,
alithibitisha kupokea maiti ya mtu mmoja ambaye inadaiwa alifariki
katika vurugu hizo.
Alibainisha kuwa walipokea majeruhi kadhaa ambao idadi yao haikufahamika na kuwa wamelazwa katika hospitalini hapo.
Naye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Stella Maris Mkoa wa Mtwara, Dk. Longino
Rutagwelela, alisema kuwa waliamua kusitisha masoma baada ya wanachuo
kuhofia hali ya usalama wao.
JK AONYA
Rais Jakaya Kikwete amesema amepata taarifa za vurugu mkoani Mtwara na
kwamba wahusika watakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Alisema wananchi lazima watambue kuwa rasilimali za nchi hii ni za watu
wote, hivyo wanaodai gesi isiende kokote hayo ni maajabu.
Rais Kikwete alisema serikali haijaisahau mikoa ya kusini ukiwamo Mtwara
kama wanavyodhani baadhi ya watu kwani ipo miradi mikubwa ambayo
imepelekwa mkoani humo.
BUNGE LASITISHWA
Bunge jana lilishindwa kuendelea na kikao cha jioni na kuahirishwa hadi
leo ili kuipa nafasi Kamati ya Uongozi wa Bunge kukaa na kuangalia
uwezekano wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwenda
mkoani Mtwara.
Hatua hiyo ilitangazwa jana jioni na Spika wa Bunge, Anne Makinda,
wakati wabunge walipoingia kuendelea mjadala wa hotuba ya bajeti ya
Wizara ya Nishati na Madini.
Aliitaka Serikali kutoa taarifa kuhusiana na tukio hilo leo asubuhi kwa
kuwa wabunge hawawezi kujadili kitu ambacho hawana taarifa za kutosha.
WANAJESHI WATATU WAFA
Habari tulizozipata wakati tunakwenda mitamboni, zilieleza kuwa
wanajeshi watatu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walifariki
dunia kwa ajali wakiwa njiani kuelekea Mtwara kwa operesheni maalum.
Habari za mitandao ya kijamii zilisema kuwa askari hao walikufa wilayani
Nachingwea wakitoka Lindi kwenda Mtwara, wengine 23 wamejeruhiwa katika
ajali hiyo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga, alisema
hana taarifa kamili za vifo ingawa alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo
na kwamba askari polisi walikua wanaelekea katika eneo la ajali.
habari nA THOBIAS MWANAKATWE
CHANZO: NIPASHE
0 comments: