Mbunge wa
Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa jana alipandishwa
kizimbani pamoja na watu wengine 76 na kusomewa mashtaka matatu kwenye
Mahakama ya Hakimu Mkazi, Wilaya ya Iringa. Mchungaji
Msigwa anashtakiwa kuhusika katika vurugu zilizotokea juzi mjini Iringa
kuhusu mgogoro baina ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na
wafanyabiashara kwenye eneo la Mashine Tatu.Baada
ya kusomewa mashtaka hayo, Msigwa ali......achiwa kwa dhamana ya Sh1 milioni
na wenzake 49 huku wengine 27 wakirudishwa rumande baada ya kushindwa
masharti ya dhamana.
Akisoma
mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa,
Godfrey Isaya, Mwendesha Mashtaka, Adolph Maganda alisema Mchungaji
Msigwa aliwashawishi watu kufanya kosa kwenye eneo la Mashine Tatu
kinyume cha sheria, kushiriki katika mkusanyiko ambao haukuwa na kibali.
Hata hivyo,
Msigwa ambaye anatetewa na Wakili wa Kujitegemea, Basil Mkwata
hakuhusishwa na shtaka jingine la kuharibu mali kwa kukusudia, ambalo
linawahusu wenzake kuanzia wa pili hadi wa 76.
Pia watuhumiwa
hao wa pili hadi wa 76, walihusishwa katika shtaka la pili la kushiriki
kwenye mkusanyiko lakini hawakujumuishwa kwenye shtaka la kwanza.Kesi
hiyo imeahirishwa hadi Juni 3, mwaka huu.
Ulinzi mkali
Mchungaji Msigwa na wenzake walifikishwa mahakamani saa saba mchana wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Mbali ya
mahakamani, ulinzi pia uliimarishwa katika Kituo cha Polisi Wilaya ya
Iringa ambako Mchungaji Msigwa na wenzake walikuwa wamewekwa.
Wafuasi wa
mbunge huyo walifurika kwenye kituo hicho na baadaye kwenda mahakamani
hali iliyowafanya polisi kuongeza ulinzi wa magari yenye maji ya
kuwasha.
Baada ya
kuachiwa kwa dhamana saa kumi na moja jioni, Mchungaji Msigwa alibebwa
juujuu na wafuasi hao ambao walimsindikiza kwa maandamano yaliyopita
barabara mbalimbali za Iringa hadi Ofisi za Chadema Mkoa wa Iringa eneo
la Mshindo.
Mbunge huyo
aliwashukuru wafuasi wake na kuwaahidi kuwa ataendelea kutetea haki zao
licha ya kufunguliwa mashtaka... “Nitawasaidia wale wote waliobaki
rumande ili kukamilisha masharti ya dhamana.”
Angalia picha zaidi hapa chini
Habari na Geoffrey Nyang’oro
Picha - Mzee wa matukio
Chanzo - Mwananchi
0 comments: