Wasomi na
Wanaharakati wamesema wangependa kuona Katiba Mpya ikipunguza nguvu ya
Kiti cha Spika wa Bunge ili kutenda haki, wakieleza kuwa inavyoonekana,
kiti hicho sasa kinaongoza kwa mabavu na upendeleo. Wakitolea
mfano wa tukio la hivi karibuni la wabunge wa Chadema kusimamishwa
kuhudhuria vikao vya Bunge kwa siku tano, wamesema,..... hawaamini kama hatua
hiyo ilifikiwa kwa haki.
Aprili
17 mwaka huu Naibu Spika Job Ndugai aliamuru askari wa Bunge wawatoe
nje ya ukumbi wabunge sita wa Chadema ambao waliwazuia askari hao kumtoa
nje Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.
Wabunge
wengine waliotolewa nje na kuzuiwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa sita
tano Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa
Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Ezekiah Wenje ( Nyamagana), na
Godbless Lema wa Arusha Mjini.
Uamuzi huo
wa Naibu Spika licha ya kupingwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
bungeni Freeman Mbowe, umeungwa mkono na Spika Anne Makinda aliyetumia
kanuni ya 2(2) na 5(1). Akitumia kanuni hizo, Spika Makinda anasema,
“Uamuzi uliofanywa na Ndugai ni halali na utaingizwa kwenye kitabu cha
maamuzi ya Spika.”
Jukata wapinga
Mwenyekiti
wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba anasema, Nguvu za
Spika katika Bunge ni kubwa mno, hivyo katiba inapaswa kuangalia upya
suala hilo na kulifanyia marekebisho.
Anasema
nguvu ya Spika ni kubwa kiasi kwamba hata Kamati ya Uongozi na Maadili
ya Bunge, haiwezi kumdhibiti kwa kuwa yeye ndiye Mwenyekiti na Naibu
wake ni Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.
“Ukifuatilia
kwa makini, Kiti cha Spika hakikutumia kanuni hata moja. Uamuzi ule
ulitungwa tu na Naibu Spika Job Ndugai na kisha kupata baraka za Spika
Makinda,” anasema Kibamba na kuongeza;
Wingi wa
wabunge wa CCM, unachangia kiti cha spika kupindisha na kukiuka baadhi
ya kanuni za Bunge katika hali inayoonyesha kutaka kuubinya upinzani.
“Ni vyema
sasa Katiba Mpya ikaweka kufuli kwa mambo makubwa yanayogusa Katiba ya
nchi ili kanuni za Bunge zisitumike kwa matakwa ya mtu mmoja.”
Kibamba
anasisitiza kuwa Katiba ijayo itamke wazi kuwa ni marufuku kwa chombo
chochote kubadilisha ibara yoyote ya Katiba kwa manufaa yao, lakini pia
mgombea binafsi wa Kiti cha Spika aruhusiwe.
“Hatua hiyo
itawapa wabunge uhuru wa kuchangia bungeni bila kuwa na hofu ya kufokewa
au kudhibitiwa na viongozi wao hasa makatibu wakuu wa vyama vyao.”
Anasema.
Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana anasema kuwa
kupindishwa na kukiukwa kwa kanuni za Bunge, kunatokana na wabunge
kujitungia na kuzipitisha kanuni hizo wao wenyewe.
“Wabunge
kujitungia na kuzipitisha kanuni zao ni makosa. Inatakiwa Katiba Mpya
itamke kwamba kanuni hizo zikishatungwa na Bunge, zihakikiwe na
kupitishwa na chombo kingine na itakuwa vizuri kama Mahakama itahusika
ili kujenga misingi bora ya uwajibikaji,” anaeleza Dk Bana.
Anaongeza
kuwa kwa mtindo uliopo sasa Bunge linajifanya kuwa polisi, mwendesha
mashitaka na Mahakama, kitu ambacho ni hatari. Lazima kifanyiwe
marekebisho kwa mujibu wa Katiba, anasema.
Dk Bana
amependekeza kuwa Katiba ijayo ije na utaratibu utakaowezesha kuwa na
kanuni za Bunge zisizofuata mfumo wa Jumuiya ya Madola. Anasema hakuna
haja ya kutekwa na Mfumo wa Mabunge ya Madola. Kinachotakiwa ni kuwa na
utaratibu mzuri wa kuendesha Bunge ili nchi zingine waige na kujifunza
kutoka kwetu.
Habari na Matern Kayera,
Chanzo - Mwananchi
0 comments: