ASKARI
Polisi Koplo Edward, anayedaiwa kusafirisha dawa za kulevya (bangi)
gunia 18 ametoroka chini ya ulinzi wa askari polisi saba na kutokomea
kusikojulikana. Mtuhumiwa huyo, alikuwa dereva wa gari aina ya Toyota
Landcruiser namba PT. 2025 la Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) Mkoa wa
Arusha. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, aliwaambia
waandishi wa habari ofisini kwake jana, kwamba askari huyo akiwa chini
ya ulinzi wa askari polisi saba, walikwenda nyumbani kwake kwa.......... ajili ya
ukaguzi.
Alisema
wakiwa nyumbani kwa mtuhumiwa, waliingia ndani kuendelea na upekuzi,
lakini katika mazingira ya kutatanisha aliwatoroka na kukimbia bila
kufanikiwa kumkamata.
Alisema kutokana na hali hiyo, polisi mkoani Arusha limemkamata Inspekta
wa Polisi Izaack Manoni aliyekuwa anasimamia upekuzi huo.
“Inspekta Manoni yupo chini ya ulinzi na hatua za kinidhamu dhidi yake zitachukuliwa,” alisema ACP Sabas na kuongeza:
“Mtuhumiwa Edward, anayetafutwa kwa sasa alishafukuzwa kazi, akipatikana
atafikishwa mahakama ya kiraia kusomewa mashitaka ya kufanya biashara
ya dawa za kulevya,” alisema.
Mei 18, mwaka huu saa 5 usiku eneo la Himo, polisi wa Kilimanjaro
walikamata gari la polisi lenye namba PT 2025, likiwa limesheheni
magunia 18 ya bangi likielekea Holili, karibu na mpaka wa Kenya.
Alisema tayari mtuhumiwa mwenzake ambaye ni askari polisi mwenye namba G. 2434 PC George, amesomewa mashitaka yake jana.
Mbali na mtuhumiwa huyo, watuhumiwa wengine waliokamatwa na magunia 30
ya bangi wilayani Arumeru nao wamepandishwa kizimbani kusomewa mashitaka
yao.
Taarifa kutoka eneo la Kwa-Morombo ilipo nyumba ya mtuhumiwa
aliyetoroka, zilidai baada ya kufika nyumbani kwake, askari saba
waliiongozana naye walimuamini na kumwacha kuingia ndani peke yake.
Ilidaiwa baada ya kuingia ndani, mtuhumiwa huyo alifungua mlango wa
nyuma ya nyumba yake na kutoroka, huku askari waliokuwa wakisimamia
upekuzi huo wakipigwa butwaa kutokumuona mtuhumiwa wao akitoka nje.
Hakuna kiongozi wa jeshi la polisi, au Serikali mkoani Mtwara ambao
walikuwa tayari kuelezea tukio hilo hadi tunakwenda mitamboni.
Morogoro
Habari kutoka mkoani Morogoro, zinasema askari polisi watatu mkoani
humo, waliokuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za kumbambikizia kesi ya
kukutwa na vufu la kichwa cha binadamu mfanyabishara Samsoni Mwita,
mkazi wa Dumila, wamefukuzwa kazi.
Taarifa iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine
Shilogile, ilisema hatua ya kuwafukuza askari hao ilifikiwa baada ya
uchunguzi kukamilika.
Alisema katika uchunguzi huo, ilibainika askari hao walikwenda kufanya
upekuzi kwa mfanyabiashara huyo, bila kuwa na kibali cha maofisa wao wa
kazi.
Aliwataja askari hao, kuwa ni mwenye namba D 4807 D/Stafu Sajenti (SSGT)
Sadick wa kituo kidogo cha Polisi Dakawa, E 4344 Sajenti (SGT) Mohamed
na E 3821 Koplo (CPL), Nuran wote wa kituo kidogo Dumila.
Alisema askari hao, walifanya tukio hilo Mei 7, mwaka huu, saa 5 asubuhi
katika kijiji cha Mgudeni, Dumila wilayani Kilosa, ambapo
walimbambikizia kesi ya kukutwa na fuvu la kichwa kinachodaiwa kuwa cha
binadamu mfanyabiashara huyo kwa lengo la kujipatia fedha.
Alisema askari hao walifanya hivyo kwa makusudi, huku wakijua kuwa ni
kosa kisheria kwa askari polisi yeyote kumbambikizia kesi raia na ni
kunyume cha taratibu, sheria, kanuni na maadili ya jeshi hilo.
Alisema katika uchunguzi uliofanywa na jeshi hilo, umebaini askari hao
wamefanya kitendo hicho kwa kushirikiana na raia Rashidi Ally (47),
mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaamu.
Awali ilidaiwa kuwa nia ya askari hao kumbambikizia kesi ya fuvu
mfanyabiashara huyo, ilikuwa kujipatia Sh milioni 25 kwa njia ya utapeli
ELIYA MBONEA, ARUSHA NA ROSE CHAPEWA, MOROGORO
chanzo - mtanzania
0 comments: